SIYO
wanafunzi tu, lakini hata watu wengi wamekuwa na dhana kwamba
mwanafunzi anayesoma sana ndiye mwenye akili nyingi na kumtabiria
kufaulu vizuri kuliko yule ambaye anasoma mara chache.
Kimantiki mtazamo huo haupingiki kwa kuwa hata kwenye suala la afya mtu akiwa mnene basi huchukuliwa kuwa ni mwenye afya njema huku mwembamba akitazamiwa kama mtu mwenye matatizo ya kiafya jambo ambalo pia huweza kuwa kinyume chake. Vivyo hivyo kwenye suala la kusoma; mwanafunzi anayesoma sana huweza kufeli na yule anayesoma mara chache huweza kufaulu, yote yanawezekana kwa kuwa kinachopima akili za mwanafunzi ni uwezo wake wa kuelewa mada alizofundishwa, kuzipambanua na kuzijibu kama mitihani yake inavyotaka.
Ukweli huu umejidhihirisha wazi mara nyingi kwenye jamii yetu ingawa sikatai kuwa wanafunzi wengi wanaosoma wanafaulu kuliko wale ambao wanasoma kwa kudonoadonoa.
Kwa mseto huu ina maana kwamba wanafunzi wengi hujisomea bila kujua wanasoma nini na wanasomaje. Kwa kifupi suala la kujisomea huhusisha mambo muhimu mawili ambayo mwanafunzi hupaswa kuyapitia ili kukamilisha mzunguko wake wa kujifunza.
Kwanza kabisa mwanafunzi hutakiwa kuandaa mada atakayoisoma kwa kutumia ‘notsi’ alizofundishwa na mwalimu wake na kutafuta vyanzo vingine vya mada husika kama vitabu au ‘material’ kutoka sehemu mbalimbali. Mwanafunzi hupaswa kusoma mada hiyo kwa kupitia vyanzo hivyo vyote huku akiandika kwa kifupi dondoo za mambo yote muhimu aliyojifunza kwa kujumlisha mawazo mengi zaidi kutoka kwa vyanzo tofauti.
Jambo la pili ambalo ni muhimu zaidi katika kujisomea ni kwa mwanafunzi huyo kujipa changamoto mwenyewe kwa kujiuliza ameelewa kiasi gani kila pointi aliyoisoma kwenye ‘material’ yote aliyokusanya kwa kupitia maswali mbalimbali kutoka kwenye mitihani iliyouliza mada husika aliyoisoma.
Kwenye hatua hii mwanafunzi huweza kujua maswali anayoweza kuyajibu na yale asiyoyaweza kiasi kwamba atapata muda wa kumuuliza mwalimu wake katika kipindi kijacho na kujiongezea uelewa zaidi kuliko wanafunzi wanaokesha wakikariri bila kufuata mbinu hizo.
Tukutane wiki ijayo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.