ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Khaa! Mbona tulikata kulia sasa? Ina maana mimi nimechanganyikiwa kiasi hicho kweli?” nilijiuliza mwenyewe.
“Basi jamani, nilikosea lakini kuna hali
inanitokea hapa ila hata nikiwaambia hamtaweza kujua,” nilisema
nikimwangalia Rehema, lakini cha kushangaza hakuwa Rehema. Alikuwa yule
mzee niliyekaa naye siti moja Dar es Salaam.
ENDELEA MWENYEWE SASA…
“Ha! Mzee we si ulishuka?” nilimuuliza nikiwa najibana kwenye kona ya siti nilipokaa.
Yule mzee alicheka sana, akaniambia: “Kijana hebu kaa kwanza. Nahisi kama umechanganyikiwa. Mimi nilishuka? Nilishukia wapi?”
Kabla sijamjibu niliwaangalia abiria wengine ili kuona kama wanatuangalia au.
Lakini walionekana wapo mbali na sisi. Kila mmoja alikuwa amekaza macho mbele kuonesha kwamba hawakuwa na habari na mambo yetu.
Nilitamani sana kuwashirikisha lakini nikawa nasita kwani hata wao sikuwaamini kwamba hawapo miongoni mwa matukio niliyokuwa nashuhudia. Yule mzee akaniambia anaamini mimi nimekanyaga jani moja ambalo linanifanya nipoteze kumbukumbu ndiyo maana najichanganya.
Nilimuuliza kama kuna jani hapa duniani ambalo ukilikanyaga mtu unapoteza kumbukumbu? Akacheka sana na kuniuliza nilizaliwa wapi mpaka niwe sijui jambo hilo.
Nilishangaa na kunifanya nianze kufikiria kwamba huenda ni kweli. Lakini ili nijiridhishe nilianza kumuuliza anakwenda wapi.
“Nakwenda Arusha, si ulishaniuliza nikakujibu. Ndiyo maana nimekwambia umepoteza kumbukumbu.”
“Unaishi Dar?” nilimuuliza tena.
“Ndiyo. Sinza, Makaburini. Nina watoto wawili. Yaani kila kitu nilikujibu, mpaka Arusha nitakaa kwa siku ngapi pia nilishakujibu, vuta kumbukumbu.”
“Unaitwa nani?”
Yule mzee akacheka sana, akasema hawezi kunijibu kwani mimi ni msumbufu sana. Nikamwomba sana, ndipo akanijibu.
“Naitwa Rahiman.”
Niliachana naye. Nikawa navuta picha ili kukumbuka kama ni jani kweli, nililikanyaga wapi kwa Dar es Salaam, tangu nitoke nyumbani hadi kituo cha mabasi cha Ubungo, sikupata jibu. Nikasema labda nililikanyaga wakati nakwenda kutafuta usafiri wa kunifikisha kituo cha mabasi.
Tulifika Korogwe sasa, ni yule mzee ndiyo aliyoniambia kwamba hapa ni Korogwe, umewahi kufika? Nikamjibu zamani sana.
“Ulifuata nini?” aliniuliza.
“Nilikuwa nakwenda Moshi.”
“Oke, sawasawa,” alinikubalia akiniangalia sana. Niligeuka kumwangalia, maana nilimjibu nikiangalia mbele, na yeye akaangalia mbele kwa haraka kama mtu ambaye hakutaka nijue alikuwa akiniangalia.
Bado mimi nilikuwa sikubaliani na yule mzee kwamba eti nilikanyaga jani ambalo liliniondolea kumbukumbu. Palepale nilishika simu na kumtumia meseji mke wangu nikimwambia:
“Nimepanda kwenye basi lakini changamoto zake kubwa sana.”
Mke wangu akaniuliza changamoto gani, nikamsimulia kwenye meseji kwa kifupi sana, akanijibu:
“Isije kuwa umekanyaga jani ambalo limekuondolea kumbukumbu?”
Nilishtuka sana, nikaangalia namba vizuri nikihisi labda aliyejibu au niliyemtumia meseji si mke wangu. Sikuamini kama mke wangu anaweza kuwiana mawazo na yule mzee kwenye basi, kivipi kwanza?!
Namba zilikuwa zenyewe lakini bado niliingiwa na wasiwasi mkubwa. Nikamuuliza mke wangu.
“Unaposema nilikanyaga jani una uhakika kuna majani ukikanyaga yanapoteza kumbukumbu?”
“We ulizaliwa wapi mpaka usijue jambo hilo? Kuna majani, miti ambayo ukiiweka chini ya nyayo unaweza kujikuta umefika hata Mwanza wakati lengo lako wewe ufike Morogoro kutoka Dar”
Mh! Niliguna, sikutegemea mke wangu aendelee kuwa sawia na yule mzee.
Wakati huo nawasiliana na mke wangu kwa simu, yule mzee alikuwa akiniangalia kwa kuibia sana asitake nijue lakini nilijua.
Basi halikusimama Korogwe, safari iliendelea na wala hakukuwa na abiria aliyeshuka. Yule mzee akasema tunatakwenda kula eneo linaitwa Mombo, nikasema wametangaza? Akajibu anavyojua yeye ni hivyo.
Mara, mke wangu akatuma meseji akiniuliza nimefika wapi katika safari yangu.
“Tumepita Korogwe lakini maruweruwe bado kwa sana kama nililivyokwambia ukasema nilikanyaga jani ndilo limenindolea kumbukumbu, umenishangaza sana kusema kuna jani limeniondolea kumbukumbu mke wangu! Hiyo ni ajabu kwangu.”
“Meseji nilituma mimi au ulitumiwa na nani? Sijakuelewa mume wangu, maajabu gani kwani umekutana nayo au nikupigie uniambie vizuri?” aliniuliza mke wangu.
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha.
Note: Only a member of this blog may post a comment.