Na Dustan Shekidele
WIVU mbaya! Mwana-ndoa Alex Bandoma anadaiwa kuchoma
moto nyumba waliyopanga huku sababu ya kufanya hivyo ikidaiwa kuwa ni
wivu wa kimapenzi kufuatia kunasa meseji aliyoamini ni ya mchepuko
iliyoingia kwenye simu ya mkewe, Sabina John (pichani).
Alex Bandoma anayedaiwa kuchoma nyumba baada ya kuhisi mkewe kuchepuka.
Tukio hilo la kushangaza lilijiri wikiendi iliyopita, saa 2:00 usiku
kwenye nyumba namba 180 waliyokuwa wamepanga iliyopo Mtaa wa Reli, Kata
ya Mazimbu mjini hapa.Mwanahabari wetu alifika eneo la tukio na
kushuhudia umati huku baadhi ya waathirika wa tukio hilo wakipekua
vyumba vyao vilivyoteketea na kukusanya mabaki ya vitu.
Nguo zikiwa zimeteketea baada ya nyumba kuchomwa moto.
Mmoja wa wapangaji hao, Upendo lssa Timbwanga aliliambia gazeti hili:
“Hawa watu kwa muda mrefu walikuwa kwenye mgogoro wa mapenzi. Kila
mmoja akimshutumu mwenzake si mwaminifu.“Kabla ya tukio, Alex alirudi
nyumbani akitokea kazini. Baada ya muda nikasikia mzozo kwenye chumba
chao, Alex akidai kunasa meseji ya mapenzi kwenye simu ya mkewe ambapo
wakati anaandaa chakula aliacha simu mezani, meseji ikaingia.
“Meseji ilisema; ‘mbona umenigandisha mpaka muda huu hujatokea au
niondoke?’ Akamwita mkewe na kumuuliza meseji hiyo ametumiwa na nani
usiku huo. ”Sabina alimjibu alitumiwa na mwanamke mwenzake jambo
lililopingwa na Alex. Wakaanza kuzozana, Alex akataka kupiga namba hiyo,
Sabina aligoma, ndipo ugomvi uliposhika kasi mpaka kutwangana
wakigombea simu hiyo.
”Lakini baada ya muda ulizuka mzozo tena kila mmoja akitaka kuchukua
tivii, deki na king’amuzi. Katika mzozo huo, Alex alivunja tivii, Sabina
akajibu mapigo kwa kuvunja deki na king’amuzi.”Upendo aliendelea kusema
kwamba, Sabina aliamua kwenda kumwita mwenyekiti wa serikali ya mtaa,
Khadija Kombo lakini akamkuta msaidizi wake, Habiba Abdallah ambaye
aliwapigia simu wajumbe wenzake na kuelekea eneo la tukio.
Mpangaji huyo alisema katika hali ya kushangaza, wakati Sabina
anahangaika kuwatafuta viongozi hao, nyuma, Alex alikuwa akikusanya
vyombo vya ndani na kuvichoma moto kwa kutumia mafuta ya taa.
Majirani wakiwa eneo la tukio.
Ilisemekana kwamba, Sabina aliporudi na viongozi hao walishtuka kuona
moto mkubwa unawaka kwenye chumba chao ambapo Alex alichomoka na
kukimbia huku moto huo ukishika kasi na kunasa kwenye paa la nyumba na
kuunguza nyumba iliyokuwa na wapangaji wanne na stoo ya kuhifadhia
vyakula.
Sabina naye, baada ya kuona nyumba hiyo ikiteketea, alimchukua
mwanaye na kukimbia kusikojulikana huku mwenye nyumba akishika kichwa
kwa mshangao.Akizungumza na gazeti hili, kaimu mwenyekiti wa mtaa huo,
Habiba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la wivu wa mapenzi
lililosababisha kuchomwa moto nyumba hiyo.
Note: Only a member of this blog may post a comment.