Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amewataka watanzania
kubeza sera za wagombea wa upinzani wanaodai kuwa serikali ya chama
hicho haijafanya kitu katika kipindi chote walichokuwa madarakani.
Akiongea katika mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi katika
jimbo la Chato ambapo ndipo nyumbani kwao, Dk Magufuli alieleza kuwa CCM
imeleta mabadiliko makubwa tangu Tanzania ilipopata uhuru ikiwa ni
pamoja na ubora wa elimu na miundombinu.
Alisema kuwa wapo wagombea ambao wamekuwa wakibeza kazi iliyofanywa
na serikali ya CCM wakati wao walikuwa mawaziri lakini hawakuweza
kujenga barabara ya lami jimboni kwao. Alisema kuwa baada ya watu hao
kumaliza muda wao, serikali ya CCM ilijenga barabara katika maeneo yao
lakini wamesahau na kukosa shukurani wawapo majukwaani.
Aliwafananisha watu hao wasio na shukurani kwa serikali ya CCM na tabia ya punda, “shukurani ya punda ni mateke.”
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli aliiwaahidi wananchi wa jimbo hilo
kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anamaliza kabisa tatizo la maji
kwa kuwa kandarasi anaefanya kazi ya kueleta maji jimboni humo
ameendelea kufanya kazi hiyo kwa kasi isiyoridhisha.
Pia, aliahidi kuwa serikali atakayoiunda itahakikisha inainua uchumi
wa watanzania wa kima cha chini kwa kuwekeza katika viwanda ili bidhaa
ghafi zinazozalishwa na wafugaji kama ngozi na kwato ziweze kutumika
katika viwanda vya Tanzania na bidhaa zitakazozalishwa ziuzwe nchi ya
nje tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa ghafi ndizo huuzwa nje ya nchi.
Alieleza kuwa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo waliopewa
walishindwa kuviendeleza, serikali yake itawanyang’anya na kuwa mali ya
serikali ili viendelee kutumika na kutoa ajira kwa wananchi.
Kadhalika, aliwasihi wananchi kuhakikisha wanalinda amani na utulivu
uliopo nchini na kutoshawishiwa na wanasiasa kujiingiza katika vitendo
vya uvunjifu wa amani.

Note: Only a member of this blog may post a comment.