MAAJABU
ya dunia! Mama wa watoto watatu, Bahati Elias (35), mkazi wa Kata ya
Ituwa jijini Mbeya anadaiwa kufufuka baada ya kufariki dunia kwa kuugua
kichwa na kifua.
Tukio hilo lilijiri Jumapili iliyopita katika Kanisa la Lulu Miracle Centre la jijini hapo ambako mwili wake ulipelekwa.
Mwanamke aliyedaiwa kufariki na baada ya maombi kuzinduka.Akizungumza na Amani kwa njia ya simu juzi, mchungaji wa kanisa hilo, Stanford Mwafulile alisimulia mkasa wa mwanamke huyo huku akisema hata yeye anamshangaa sana Mungu.
“Siku hiyo asubuhi, walikuja watu kanisani kwenye ibada, wakaniambia kuna mwanamke anaumwa, hali yake si nzuri, anatapatapa, wakaniomba niende kwake nikamwombee.
“Nilikubali, nikawaambia watangulie. Lakini kabla sijatoka, akaja mtoto akaniambia yule mgonjwa amefariki dunia.
“Mimi niliwaambia waubebe mwili waulete kanisani maana si mbali. Wakafanya hivyo. Naamini lilikuwa tukio la kukusudiwa na Mungu ili apewe utukufu.
“Mwili uliletwa, nikasitisha ibada. Mimi na wasaidizi wangu tukaanza kuuombea kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa saba mchana, akazinduka. Nilifanya vile kwa sababu niligundua nafsi ya marehemu ilifichwa ila mwili wake ndiyo ulipoa lakini uhai ulikuwa ungalimo ndani mwake. Alipofufuka, mimi nilikuwa wa kwanza kulia,” alisema mchungaji huyo.
Aliendelea kusema kuwa, wakati maombi yakiendelea, walifika mashemeji wa marehemu na kuutaka mwili huo wakauzike kwa vile alishafariki dunia tangu asubuhi, yeye mchungaji akawagomea.
Akizungumza na Amani baada ya kupelekwa nyumbani kwake kuoga na kurudi tena kanisani hapo, mwanamke huyo alisema hana cha kuongeza bali anampa utukufu Mungu kwa maajabu yake.
Kwa upande wake, Mchungaji Mwafulile alisema Bahati aliachwa na mumewe na watoto wake watatu anaowalea kwa sasa, Irene, Bry na Jack.

Note: Only a member of this blog may post a comment.