Friday, September 4, 2015

Anonymous

KERR wa SIMBA SC: Nitaweka Rekodi Ligi Kuu

o7bkHdw7

Kocha wa Simba, Dylan Kerr.
Martha Mboma na Omary Mdose
WAKATI Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kuanza Septemba 12, 2015, tayari tambo zimeanza kuwa nyingi huku Kocha wa Simba, Dylan Kerr akijinadi kuwa amepania kuivunja rekodi ya timu yake kutoshinda kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Simba imekuwa ikipata wakati mgumu uwanjani hapo kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, bila kujali inacheza na timu ipi katika ligi kuu.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Simba itafungua pazia uwanjani hapo kwa kukipiga na African Sports ambayo imepanda daraja hivi karibuni, kisha itabaki Tanga kukipiga na Mgambo JKT kwenye dimba hilohilo.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Kerr alisema hana hofu juu ya uwanja huo wala hatishwi na rekodi ya timu yake kutofanya vizuri uwanjani hapo.
“Sijawahi kucheza uwanjani hapo lakini hiyo hainipi hofu na malengo yangu ni kuweza kuvunja hiyo rekodi mbaya ya kutofanya vizuri kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri kwa michezo yake yote ambayo itacheza hapo.

“Ni vizuri kuanza ligi vema kwa kuwa na matokeo mazuri ambayo yatawapa nguvu zaidi ya kujituma na kufanya vizuri, nina wachezaji wazuri ambao wanajua nini wanafanya, hilo nalo litanisaidia kwa kiasi kikubwa,” alisema Kerr.

Rekodi zinaonyesha matokeo ya Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani kwa misimu mitatu iliyopita yalikuwa hivi: 2012/13, Coastal Union 0-0 Simba, Mgambo 0-0 Simba. Msimu wa 2013/14, Mgambo 1-0 Simba, Coastal Union 0-0 Simba, Msimu wa 2014/15, Mgambo 2-0 Simba, Coastal Union 0-0 Simba.
Upande wa Yanga uwanjani hapo rekodi zipo hivi: 2012/13, Coastal 0-2 Yanga. 2013/14 Mgambo 1-0 Yanga, Coastal 0-0 Yanga. 2014/15 Mgambo 0-2 Yanga, Coastal 0-1 Yanga.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.