
Siku 2 ndani ya Mkoa wa Tabora mbali ya kuendelea kusikia na kujionea kilio cha wakulima, lakini pia zimeongeza ari niliyonayo ya kuhakikisha kilimo chetu kinawanufaisha wakulima wenyewe kwa kuwaongezea kipato na kuboresha maisha yao na hatimaye ustawi na maendeleo ya nchi nzima.
Kupuuza wakulima kama inavyofanyika sasa hivi ni kuchagua kushindwa.
Wakulima wa Tumbaku mkoani Tabora kama ilivyo kwa wakulima wa maeneo mengi nchi nzima wanaolima mazao ya biashara hata na yale yachakula, wana kilio kikubwa cha kukopwa. Wanakopwa hadi na serikali iliyotakiwa kuwasaidia au kuweka mazingira bora ya wakulima kupata thamani ya kile wanachozalisha. Mkulima wa Tumbaku huko Sikonge au Urambo au Kaliua na maeneo mengine wana simulizi za kusikitisha namna wanavyohangaika kuzalisha lakini hawanufaiki inavyowastahil.
Nimewahikikishia wananchi wa Mkoa wa Tabora ambao asilimia kubwa wanaishi kwa kutegemea zao la Tumbaku, masuala kadhaa.
1. Serikali nitakayoiunda hapo Novemba mwaka huu baada ya Watanzania kunichagua na kunikabidhi dhamana ya uongozi mkuu katika nchi, haitaruhusu wakulima wa tumbaku kukopwa kama ambavyo inafanyika sasa.
2. Suala la manyanyaso ya kupata pembejeo litakuwa historia. Nitalighulikia lisiendelee kuwa kikwazo katika kuhakikisha wanazalisha kadri ya uwezo wao kujiongezea kipato lakini pia kujitajirisha.
3. Serikali yangu itaweka mazingira rafiki ili kutengeneza fursa za wakulima kuuza mazao yao kokote kule wanakotaka kadri ya soko linavyohitaji.
4. Wale wote waliohusika katika kuwakopa wakulima wa tumbaku nimewapatia muda hadi Oktoba ndiyo salama yao. Walipe madeni yote ya wakulima hao. Ikifika Novemba nami nikiwa ikulu kwa kura za Watanzania, sitakuwa na maneno tena kwa wahusika. Watalazimika kuwalipa wakulima mara mbili ya kiwango wanachodai sasa.

Note: Only a member of this blog may post a comment.