Saturday, September 12, 2015

Anonymous

JB Pamoja na Kupata Fedha, Umaarufu Wamtesa!

JB
MAISHA ni safari ndefu iliyojaa kila aina ya hali. Imejaa milima na miinuko mikali, mabonde, miiba, dhoruba na tufani kali. Hakika ni watu waliodhamiria tu kutafuta mafanikio ndiyo huweza kuhimili vishindo na misukosuko ya safari ya kutafuta mafanikio maishani.
Kila aliyefanikiwa kwa njia halali, nyuma amepitia mapito mengi magumu na makali mno. Upo msemo ambao binafsi kila nikiukumbuka, morari na nguvu ya kutafuta mafanikio maishani huongezeka maradufu.

Msemo huo unasema; Every successful person has a painful history and every painful history, has a successful ending (Kila binadamu aliyefanikiwa, ana historia yenye maumivu na kila historia yenye maumivu, huwa na mwisho wenye mafanikio).

Hayo ndiyo maisha. Hakuna kilicho chema ambacho hutokea kwa njia rahisi. Hakuna. Jasho, machozi, maumivu na wakati mwingine hata damu, huhitajika kukamilisha gharama ya mafanikio.

Cha muhimu ni kuwa na ndoto, kujiwekea malengo, kuamini kuwa inawezekana na kisha kuchukua hatua kufuatilia ndoto ya maisha yako. Hakuna njia rahisi zaidi ya kupambana huku ukimtanguliza Mungu kama nguzo muhimu ya safari yako.

JB, ambaye kwa hakika ni staa mkubwa wa filamu Bongo, anayo simulizi ya kusisimua kuhusu maisha. Anasimulia na kueleza hatua kwa hatua namna na jinsi ambavyo ameweza kufika hapo alipo katika maisha. Hakika ni simulizi ambayo hata mimi ninayeandika, imebadilisha kabisa maisha yangu.

Wiki iliyopita, alieleza jinsi alivyolazimika kuachana na msambazaji wake wa kwanza wa Kampuni ya Wananchi Store, Farhaji Mohamed na kuungana na kampuni ya Steps Entertainment, baada ya kushawishiwa na msanii mwezake, Vincent Kigosi ‘Ray’ huku wingi wa pesa alizoahidiwa ukichangia kwa kiasi kikubwa. Je, nini kitaendelea? Kanyaga twende….

“Tayari akili yangu ikawa haiwazi kitu kingine zaidi ya pesa, sasa nilishaamua kufanya kazi ya uigizaji kama ndiyo maisha yangu, moyoni nikajiapiza kuifanya kwa uadilifu na nidhamu kubwa mno,” anaendelea kusimulia JB.

Haraka sana JB ananigusa kwenye paja la mguu wa kushoto na bila kuchelewa akanikazia macho na kusema: “Siku zote katika maisha, jitahidi sana kukipenda na kukiheshimu kile kinachokufanya uendelee kuishi, hapo namaanisha kazi,” anasema JB na kuuondoa mkono wake pajani kwangu na kuifuata chupa yake ya maji.

“Kwa hiyo nikawaita waigizaji ambao nilikuwa nao, nikapandikiza mbegu ya ushindi kuwa kwa sasa ilikuwa ni kupambana tu, hakuna lelemama, huwa sina mchezo wala masihara linapokuja suala la kazi. Sina,” anasema JB huku akitazama juu na kukunja ndita mithili ya mbogo jike aliyenyang’anywa watoto wake mwituni.

“Baada ya hapo, nikatengeneza sinema ya Zawadi ya Birthday ambayo nilishirikiana na Richie, lakini pia ni sinema ambayo ilimuibua kwa kasi sana muigizaji wa kike ambaye kwa hakika kwa sasa anafanya vyema mno, Shamsa Ford ‘Chausiku’,” anasema.

“Baada ya hapo, nikatengeneza tena sinema inaitwa Senior Bachelor, baada ya hapo ikaja Dj Ben, baadaye Dereva Taksi, Danija, Mzee wa Swagga na nyingine nyingi mno ambazo zimeanza kunitoka, lakini acha niwe mkweli katika hili mdogo wangu,” anasema JB kwa sauti ya kukatakata.

“Mmh,” najikuta nikimuunga mkono kwa kuitikia kwa mguno huku akili na mawazo yangu yote yakiwa kwenye kitabu changu cha kuandikia, nadondosha wino kwa madaha kwa kuwa kuandika ndiyo kazi ninayoipenda kuliko zote maishani.

“Kati ya sinema zote ambazo binafsi nimeigiza, hakuna filamu ambayo niliitendea haki kama Senior Bachelor, hakika niliigiza kwa kiwango ambacho kila nikiitazama huwa namshukuru Mungu kwa kipaji hiki,” anasema JB kwa hisia kali sana.

“Lakini wapo wengine huniambia hakuna sinema kali niliyowahi kuigiza kama Dj Ben, wengine Dereva Taksi, basi ilimradi mashabiki ndiyo mahakimu wangu katika kazi,” anasema.

“Kufikia hapo, umaarufu ukaanza kuongezeka sana, nikaanza kuishi maisha ya umaarufu ambayo kwa kweli yanatesa sana, huwezi kuwa huru, ukipita mahali kila mtu anakukodolea macho, kwa kweli hakuna maisha magumu sana kama ya umaarufu,” anasema.
“Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea, kuna jambo nimesahau kukueleza, ngoja nikuambie,” anasema JB na kujitengeneza vyema kwenye kiti nami nakaa mkao wa kusimuliwa zaidi.
Je, nini kitafuata? Ni jambo gani JB anataka kusema? Usikose kufuatilia wiki ijayo kwa uhondo zaidi. Tchao.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.