Mariamu akionesha jeraha lililopo mbavuni.
UMAFIA wa kutisha! Dada mmoja
aliyefahamika kwa jina la Mariamu mkazi wa Mwananyamala jijini Dar,
amefanyiwa umafia kama siyo unyama wa kutisha na bosi wake aliyekuwa
akimfanyia kazi za ndani.
Mariam aliliambia gazeti hili juzi kuwa, tukio hilo lilitokea usiku
wa Jumapili ya Septemba 13, mwaka huu nyumbani kwa bosi wake huyo
aitwaye David maeneo ya Kinondoni jijini Dar.
Msikie Mariam
“Ilikuwa ni kawaida yangu kila Jumapili kwenda nyumbani kwake
kumfanyia shughuli za usafi kwa malipo ya shilingi 10,000 mara nyingine
15, 000 sasa tofauti na siku zote, Jumapili hii nilipokwenda nilimkuta
akiwa na mgeni aliyenitambulisha kuwa ni mdogo wake.
“Nikiwa kwenye sherehe, bosi wangu huyo alinipigia simu na kunitaka
nirudi maana kulikuwa na upotevu wa simu. Nikamjibu kuwa sijaichukua
mimi lakini hakunielewa, ndipo nikaamua kwenda nyumbani kwake.
Alipofika ikawaje?
“Nilipofika alinichukua yeye na mdogo wake na kuanza kunishambulia
kwa kunipiga na mabapa ya panga huku akinitaka nioneshe mahali
nilipoificha simu hiyo. Nilizidi kujitetea kuwa sikuchukua lakini
hakunielewa, akazidi kunitesa.
“Akaniingiza kwenye chumba f’lani na kunivua nguo kisha akawa
ananipiga kwa bapa la panga ambapo alinikata mgongoni. Wakachukua pasi
yenye moto na kunichoma sehemu mbalimbali mwilini, walinitesa sana.”
Apata upenyo
“Kuna wakati waliniacha kwenye chumba hicho ndipo nilipowapigia simu
ndugu zangu na kuwataka waje haraka ikiwezekana na polisi. Hata hivyo,
walishindwa kuwapata polisi ila walikuja wenyewe na kunikuta
nimeshatolewa nje na kuambiwa niondoke haraka.
Breki ya kwanza polisi
Mariamu alizidi kueleza kuwa, kutokana na hali aliyokuwa nayo ndugu
zake walimshauri kwenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Oysterbay.
“Tulienda pale polisi Oysterbay, tukaandika maelezo kisha tukapewa
fomu kwa ajili ya matibabu (PF3) na kufungua RB yenye namba:
OB/RB/14593/2015, KUJERUHI kisha nikaenda hospitali ambako nilitibiwa
ikiwa ni pamoja na kushonwa nyuzi 18 mgongoni na 16 mkononi,” alisema
Mariam.
Jitihada za kumpata mtuhumiwa huyo hazikuzaa matunda ila taarifa za kipolisi zimethibitisha kukamatwa kwa bosi huyo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.