Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ni waandaaji wa Miss
Tanzania, Hashimu Lundenga amesema kuwa baada ya Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) kulifungulia shindano hilo, sasa wana kazi kubwa ya
kurudisha imani kwa mashabiki na wadhamini.
“Sisi kama Lino International Agency Ltd tumepokea taarifa za
kufunguliwa kwa mashindano ya Miss Tanzania kwa furaha sana, mashindano
haya yalifungiwa kwa miaka miwili sasa kufunguliwa kwa mashindano haya
baada ya miezi saba au nane ni jambo kubwa sanaa, hivyo tumekubaliana na
BASATA na tumepewa kibali cha maandalizi ya awali tunajua tumepoteza
nafasi nzuri kwa wadhamini hivyo itatupa kazi kubwa kidogo kujijenga na
kurudisha imani kwa wadhamini wetu tena,” alisema Lundenga.
Akiongea na East Africa Radio, Ludenga amekiri kuwa kutokana na
kujihusisha na mashindano hayo kwa muda mrefu kuna uwezekano watu
wanahitaji kuona mabadiliko, hivyo wanampango wa kuweka kamati mpya
itakayokuwa na watu wapya.
“…Inawezekana watu wamechoka sababu sisi tupo katika mashindano
haya kwa miaka ishirini iliyopita hivyo tunakubali watu wametuchoka
hivyo sisi wawili watatu hatutakuwa mstari wa mbele katika kamati hizo
bali tutakuwa na kamati mpya ambayo itakuwa na watu wapya, maana watu
wametuchoka hivyo lazima waje watu wapya wenye mawazo mapya na ndiyo
watakuwa mstari mbele, hiyo itatusaidia kujua tumekosea wapi.”
Chanzo: Eatv.tv

Note: Only a member of this blog may post a comment.