Mwigizaji mkongwe wa filamu nchini Natasha Mamvi amesema utovu wa
nidhamu na maisha yaliyojaa ukakasi kwa waigizaji wa kike hivi sasa, ni
matokeo ya kuingia katika fani pasipo kupitia mafunzo ya taaluma hiyo.
“Kile kitu ambacho unakiona ni kinyume na filamu, ujue huyo mtu hajapita katika mafunzo,” alisema. “Zamani kila tulipoingia kwenye makundi, kitu cha kwanza kabisa ilikuwa tunafundishwa nidhamu kama msanii na kama mtoto wa kike.
“Tulikuwa na watu wazima ambao walikuwa wanatuangalia na kutushauri au kukataza tabia fulani. Ilikuwa ukifanya kitu unaambiwa aah hicho kiache wewe ni msanii kioo cha jamii.”
Anasema kwa kuwa wengi hawajapata mafunzo hayo, yanayotokea sasa ni majibu ya kile ambacho kiliharakishwa kwa kisingizio cha kuwa na kipaji. “Kwa sababu wengi hawajapita katika mafunzo kama hayo, ndiyo maana leo hii haya yote yanatokea. Kuvaa nguo zisizo na staha, kuzungumza maneno yasiyo na staha, kukaa kwenye maklabu mpaka saa mbaya na hata kutengeneza skendo, ni vitu ambavyo unaona kabisa kwamba huyu mtu amekosa mafunzo,” alisema.
Natasha alisema awali wasanii walikuwa wakipitia kwenye vikundi na kujifunza misingi ya sanaa, tofauti na ilivyo sasa.
“Kwa mfano hivi sasa ukimchukua mtu ukaenda naye location (eneo la kuchukulia picha za filamu) unaweza kushangaa huyu ni msanii maarufu lakini mbona ABC hazijui? Na ukimwambia kwamba anakosea anakuwa mkali. Basi unamwangalia tu,” alisema.
“Nakumbuka kuna kipindi chipukizi waliniita kwa ajili ya kutengeneza filamu. Nikamuona mpigapicha anakosea kuchukua picha, nilipojaribu kumwambia akanuna. Nikashangaa kwa kuwa mimi nimekaa muda mrefu kwenye sanaa nilihitaji kumfahamisha lakini hakunielewa. Hapa ndiyo unaona aah kumbe kutokuingia kwenye vikundi au kupata yale mafunzo ya mwanzo kunasumbua tasnia yetu.”
Natasha, ambaye jina lake halisi ni Suzan Lewis, anafafanua kwamba ndiyo maana leo hii waigizaji wa kike wanajiachia hadharani bila kujali nini wanafanya na hata kutumia vibaya ya mitandao ya kijamii.
Anasema bado hajafanikiwa kuwapa elimu ya namna ya kujichunga.
“Hicho ni kitu ambacho sijawahi kukaa na kuzungumza nao. Siyo kitu cha kistaarabu. Wewe kama mwigizaji wa kike lazima ujue kwamba una wafuasi wangapi katika ukurasa wako wa mtandao wa kijamii. Lazima ujijue kwamba wewe ni maarufu na ujue kwamba unachokiandika kinamfikia nani na kitawavutia vipi watu au kuwakera.
“Mtu unaweza ukaandika mambo poa, mtu anaanza kujiuliza mambo poa ile ishu ya jana. Yaani neno dogo lakini kila mtu atatafsiri kitu chake, lakini unaweza kukuta mtu anakurupuka na kuandika kitu mtandaoni mpaka ukashtuka. Jaribu kuangalia mara mbili kile kitu unachoandika kina manufaa gani, siyo kitu cha kufundishwa ila ni umakini wa mtu mwenyewe,” alisema Natasha.
Chanzo:Mwananchi

Note: Only a member of this blog may post a comment.