Hamida Hassan na Mayasa Mariwata
UKATILI wa mume! Mama mmoja, Neema Mwita
aliyeripotiwa na gazeti hili kuwa aliunguzwa na uji wa moto na mumewe
Juma Mwita, amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar
es Salaam.
Mama
huyo baada ya kumwagiwa uji na kulazwa takriban mwaka mzima kwenye
Hospitali ya Mkoa wa Mara na kushindikana kupona, hivi karibuni aliletwa
Muhimbili na Mtangazaji wa Kipindi cha Wanawake Live, Joyce Kiria
ambapo amelazwa kwenye Wodi Namba 24, Jengo la Sewa Haji.
Akizungumza kwa tabu mama huyo alisema kuwa licha ya kupata kilema
cha maisha, anamshukuru Joyce na gazeti hili na wote waliojitokeza
kumsaidia kwani hatua aliyofikia sasa inaridhisha na atapona kwani
amefanyiwa upasuaji baada ya kuondolewa nyama kwenye paja.
Neema alipatwa na janga hilo baada ya kuchuma mahindi shambani
kitendo kilichomchukiza mumewe aliyeamua kumuunguza kwa uji uliokuwa
umeandaliwa kwa ajili ya kusongea ugali.
“Naomba msaada kwani ndugu zangu hawana uwezo, licha ya kwamba Napata
chakula cha hospitali kuna huduma nyingine zinahitaji fedha,” alisema
mama huyo.
Kwa yeyote anayependa kumsaidia mama huyo awasiliane naye kwa namba ya simu 0656151072 au 0756768305, kutoa ni moyo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.