Saturday, August 1, 2015

Anonymous

SHTUKA! Pesa zako zinaishia kwenye sherehe, hivi umerogwa au?!

Hakuna ubishi kwamba wanawake wanaongoza kwa kuendekeza sherehe kuliko wanaume. Ukifuatilia sana utagundua kuwa, wanaume si watu wa kupenda sana mambo hayo ila wakati mwingine wanalazimishwa kushiriki.

Mifano iko mingi huko mtaani, unaweza kukuta mke anataka kufanya sherehe ya mtoto kutoka arobaini lakini mume anaona haina haja, matokeo yake wanatofautiana.

Nikiri tu kwamba hakuna mtu asiyependa sherehe lakini wakati mwingine tunatakiwa kuangalia sherehe za kutuumiza akili zetu. Wapo watu ambao hakipiti kipindi kirefu lazima utasikia wana sherehe. Sawa hatukatai hizo sherehe zenu lakini zina ulazima kufanyika?

Kweli kuna ulazima wa kutumia mamilioni ya fedha kuwaita watu waje kula, kunywa na kucheza muziki wakati kuna mambo mengi ya msingi ya kufanya yanayohitaji hizo pesa?

Nasema hivyo nikiwa na mifano hai. Yupo mama mmoja ambaye ni jirani yangu, yeye anaishi kwenye chumba cha kupanga na biashara yake kubwa ni kuuza samaki.

Mama huyu anapata pesa nyingi lakini cha ajabu, kila wiki lazima aende kwenye sherehe. Anatumia pesa nyingi kutoa michango na siku ya tukio lazima anunue sare.

Sasa unajiuliza kwamba, ina maana ile ungua na moto yote kwenye biashara yake ya samaki ni kwa ajili ya sherehe? Kwamba hana mambo ya maana ya kufanya kwa faida anayopata?

Siyo huyo tu, wapo wanawake wengi wenye tabia hiyo. Wanahenyeka kusaka pesa lakini wakizipata zinaishia kwenye sherehe. Yaani wasiposhiriki kwa kutoa michango au kununua sare hujisikia vibaya sana.

Mbaya zaidi ukiwaangalia maisha wanayoishi ni ya kifukara. Ni wagumu kwenye kulipia ada za watoto wao, kuwalisha watoto wao chakula kizuri au kuwanunulia nguo nzuri lakini wasikose pesa ya kununua sare ya harusi. Watu wa dizaini hii wamerogwa au kitu gani?

Kama nilivyosema hapo awali kwamba, hukatazwi kushiriki kwenye mambo ya kijamii kama hayo lakini usiyaendekeze sana. Wengi ambao wameendekeza mambo hayo wamebaki kuishi maisha ya kawaida na hata faida ya kufanya biashara zao hawaioni.

Wapo wanawake wengine wanafanya kazi zao za kutafuta pesa kisha wanacheza michezo ‘upatu’ lakini ikifika zamu yao ya kupokea pesa zinaishia kwenye mambo ya ajabu. Lini utafikiria kufanya mambo ya kimaendeleo?

Nimewagusa sana wanawake kwa kuwa ndiyo wanaoonekana kuweka mbele mambo ya sherehe na kutumia pesa nyingi.

Wapo ambao hufikia hatua ya kutibuana na waume zao kisa wameomba pesa za mchango wa shughuli ya jirani na mwanaume akakataa.

Naomba niseme kwamba, ukimuona mwanaume anakataa kukupa pesa kwa ajili ya mchango wa sherehe ya rafiki yako au kwa ajili ya kununulia sare usidhani ni bahili. Tambua anajua madhara ya kuwa muumini wa kutoa pesa kiholela kwa ajili ya sherehe.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.