Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) ameanza kuonja joto la kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya watu wanane kujitokeza kwa siku ya kwanza kuitaka nafasi hiyo.
Kati ya waliojitokeza kuwania ubunge kupitia CCM ni mtoto wa waziri mkuu wa zamani Joseph Warioba, Kipi Warioba na Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jumaa Mhina ‘Pijei’.
Pia yumo Elias Nawela, Dk Walter Nnko, Atulinda Barongo, Tegemeo Sambili, Shuganga George na Edmund Lyatuu.
Mdee amekuwa mbunge wa jimbo hilo
kupitia Chadema tangu mwaka 2010, lakini sasa atakuwa na kazi ya
kupambana na baadhi ya makada hao wa CCM waliochukua fomu kulitaka jimbo
hilo.
Wengine katika maeneo mbalimbali nchini
waliochukua fomu ni pamoja na Moshi Mjini ambako makada wa CCM wameanza
kupigana vikumbo kutaka kumrithi mbunge wake wa sasa, Philemon Ndesamburo.
Kada wa kwanza aliyechukua fomu ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Mwita na wafanyabiashara, Davis Mosha na Patrick Boisafi.
Mjini Mbeya, Mwenyekiti wa UVCCM, Amani Kajuna ameibuka na kutaka kuwania ubunge Jimbo la Mbeya Mjini.
Katika Jimbo la Kinondoni Idd Azzan anayetetea jimbo lake anatarajiwa kuchuana na Wangota Salum, John Kalinjana na Goochange Msangi wakati Ubungo Didas Masaburi na Joseph Massana wamejitokeza kumvaa John Mnyika.
Katika Jimbo la Kibamba waliojitokeza ni George Shija, Dk Meshack Sabaya, Dk Fenella Mukangara na Rashid Kikazi.
Wanaowania kupitia viti maalumu Kawe ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Angela Kairuki, Zarina Madabida, Getrude Lwakatare, Florence Masonga,
Mary Daffa, Warda Maulid, Anna Matulu, Emelda Mwananga, Maria Kigalu,
Angela Kizigha na Ummy Nderiananga.
Mkoani Dodoma, mbunge anayemaliza muda wake, David Malole na anayemiliki Kiwanda cha Magodoro ya Dodoma asili, Haidari Gulamali wamejitokeza kuchukua fomu pia.
Jimbo la Chilonwa waliojitokeza ni pamoja na Joel Makanyaga, Daniel Ligoha, Anderson Magolola, Deo Ndejembi na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Pololeti Mgema na Dk Kedimon Mapana.


Note: Only a member of this blog may post a comment.