Ukitaka kujua afya yangu, mimi pia namshukuru Mungu. Naendelea na majukumu yangu kama kawaida. Nimekukumbuka leo kupitia barua, nina jambo nataka nitete na wewe kidogo.
Wiki iliyopita Watanzania wenzangu tulifurahi kupata habari njema. Kwamba yale mashindano ambayo wewe ulikuwa ukiyaratibu kwa kipindi kirefu ya Miss Tanzania, yamefunguliwa kutoka kifungoni.
Nilifurahi zaidi baada ya kuona barua yao ya kukuruhusu uendelee kwani Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) waliokufungia, waliainisha kuwa, wamekuruhusu kuendelea baada ya wewe kuomba radhi na kufanyia kazi upungufu ulioonekana katika shindano lako.
Nikiwa kama mdau wa burudani, ninayependa kuyaona mashindano hayo yakiwa na umri mrefu na kuleta tija kwa nchi yetu, nakusihi ndugu yangu, usiturudishe tena kule tulikotoka. Usiturudishe kule kulipokuwa kunalalamikiwa na Watanzania.
Nakuomba sana, weka utaratibu mzuri ambao hautakuwa na maswali wala kuleta manung’uniko. Mshindi apatikane kihalali. Kila mtu aone kweli huyu alistahili kuwa Miss Tanzania. Sheria zinazotakiwa katika mashindano hayo zifuatwe, kusiwe na ubabaishaji.
Tunatamani kuona mrembo anayezaliwa kutoka kwenye shindano lako, anatuwakilisha katika mashindano ya dunia na kushinda. Tumpitishe mtu ambaye atakuwa na sifa na vigezo vya kushiriki mashindano ya dunia.
Sitaki kukumbushia yale yote ambayo kipindi cha nyuma yalikuwa hayaendi sawa lakini ninachotaka kukwambia, simamia weledi kuanzia sasa na kuendelea. Watanzania wanatambua upungufu uliokuwa ukitokea kwenye mashindano hayo lakini pia wanatambua mazuri mengi uliyokuwa ukiyafanya.
Naamini umepata muda mzuri sana wa kuyaboresha mashindano katika kipindi hiki cha zaidi ya mwaka mmoja ulichokuwa umefungiwa. Umeshafanya utafiti wa kutosha na kujua unachopaswa kukifanya ili Watanzania wapate burudani nzuri kupitia mashindano hayo.
Nikiwa kama mdau wa burudani, natambua umuhimu wa mashindano hayo. Natambua faida yake si tu kwa mshindi mmojammoja bali hata kwa taifa. Anapopatikana mshindi, akafanya shughuli mbalimbali ndani na nje ya nchi, anaitangaza Tanzania. Anatangaza utalii wetu kwa wazawa na mataifa mengine.
Tuamue kwa nia ya dhati kuyafanya yawe na hadhi na ninawaomba Watanzania waendelee kukuunga mkono. Watakuunga mkono kama hakuna longolongo. Naamini umejipanga, basi fanya kweli. Tunataka kuona ubora ule wa miaka ile iliyowatoa warembo kama kina Hoyce Temu, Jacqueline Ntuyabaliwe, Angela Damas na wengineo.
……………
Erick Evarist


Note: Only a member of this blog may post a comment.