KWA jina naitwa
Mussa (anaomba ajulikane kwa jina hilo). Ni mkazi wa Sinza Makaburini
(Dar). Nina mke na watoto wawili. Mmoja anasoma Shule ya Msingi
Mashujaa, mwingine anasoma Shule ya Msingi Reginald Mengi. Nimekuwa
nikisoma mikasa mingi ya watu kupitia mtandao huu wa www.kandiliyetu.com kwa muda mrefu sasa.
Kutokana na kusoma mikasa hiyo, nimeona na mimi nitoe mkasa wangu. Huu mkasa ulinitokea ndani ya basi moja (anaomba asilitaje jina) linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam mpaka Arusha.
Anaendelea: Ilikuwa Januari, mwaka huu. Nilipata safari ya kikazi kwenda Arusha mjini kwa ajili ya kufuatilia malipo kwenye kampuni moja tuliyofanya nayo biashara miezi mitatu nyuma.
Safari ilianza saa kumi na mbili na nusu asubuhi au niseme alfajiri. Siti yangu ilikuwa namba 34 upande wa dirishani kwenye upande wa dereva.
Abiria tulitangaziwa kufunga mikanda, mimi nilifanya hivyo haraka sana ili kuwa salama zaidi. Abiria niliyekaa naye siti moja alikuwa mzee mmoja hivi, yeye alisema hawezi kufunga mkanda kwa sababu utambana sana.
Basi lilipofika Mbezi Mwisho, lilisimama kupakiza abiria. Huyu abiria wakati anaingia nilimwona. Ni msichana aliyevaa gauni jeupe, refu. Chini alivaa viatu vya ngozi, vyeusi na alibeba mkoba mdogo tu.
Sikumfuatilia kujua anakwenda kukaa wapi kwani alipoingia tu, mimi nilipindua macho na kuangalia nje.
Safari ilianza huku mimi nikiendelea kuangalia nje. Nilikuwa nikiangalia mazingira ambayo kwangu ni mageni katika Jiji la Dar es Salaam. Niliona majumba mengi ya kifahari mpaka nikawa nashangaa mwenyewe.
Muda wote huo, macho yangu yalikuwa nje kuanzia hapo Mbezi. Nilikuja kushtuka baada ya basi kuingia Maili Moja, Kibaha. Nikarudisha ufahamu wangu kuangalia ndani ya basi.
Jambo la kwanza lililonishangaza ni kumwona abiria mwenzangu niliyekaa naye tangu Dar si yule mzee, bali ni yule msichana aliyepandia Mbezi Mwisho. Nilishtuka sana.
Nikamwangalia usoni, akaachia tabasamu na kunisalimia.
“Mambo vipi anko?”
Nilimjibu poa, lakini uso wangu ulikuwa na maswali kibao. Yule mzee alishukia wapi na muda gani! Nilitembeza macho siti za mbele, nikarudi hadi siti za nyuma nikimwangalia yule mzee kwamba huenda alihama siti. Lakini kumbukumbu yangu iliniambia kwamba, tangu tunatoka Dar hakuna siti iliyokuwa wazi.
“Hapa kulikuwa kuna mzee amekaa tangu Dar. Hujamuona?” nilimuuliza yule msichana.
Alikuwa msichana mzuri kwa sura, umbo na hata mwonekano wote kwa ujumla. Kabla hajanijibu, aliachia tabasamu laini kwanza kisha akasema:
“Hapana anko. Sijamwona.”
“Na wewe wakati unapanda pale Mbezi kuna abiria alishuka?” nilimuuliza swali la pili.
“Hapana anko, hakuna abiria aliyeshuka.”
Niliogopa sasa. Haikuwa hali ya kawaida. Niliishiwa nguvu. Nikamwangalia abiria mwingine aliyekaa siti sanjari na siti yetu kushoto kwangu. Yaani baada ya yule msichana inayofuata korido ya basi halafu yeye.
“Eti bro, hapa si nilikaa na mzee mmoja. Unakumbuka?”
“Hapana, sijafuatilia. Alipandia tangu Dar?”
“Ndiyo.”
“Sijamwona. Mimi nimemwona huyu mrembo tu.”
“Tangu Dar?” nilimuuliza.
“Kwani tatizo lako liko wapi ndugu? Hutaki kukaa na abiria wenzako au?” yule mtu alinijia juu, nikanyamaza.
Wakati narejea kukaa sawasawa kwenye siti, niliwaangalia abiria wengine, wote walionekana kuwa bize na kuangalia mbele ambapo kulikuwa na tivii ikionesha filamu ya kutisha.
Filamu ile ilikuwa ni ya abiria wakiwa ndani ya basi wakitoka sehemu moja kwenda nyingine. Sasa ndani ya basi lao aliingia mnyama ambaye mimi sikumjua kwa jina wala sikuwa na uzoefu wa kumuona popote pale. Hata kwenye vitabu.
Na mimi niliiangalia filamu hiyo lakini nikaona kama inanitisha, nikaachana nayo kwani yule mnyama alikuwa akila abiria mmojammoja na sasa alikuwa anakaribia kwa dereva.
Basi, nilikaa kwa machale sasa. muda mwingi nilikuwa nikimwangalia yule msichana ambaye naye muda mwingi alionekana kuniangalia mimi kwa kuniibia.
“Anko samahani,” alinitaka radhi, nikamwangalia.
“Unaitwa nani?”
“Mimi naitwa Frank,” nilimjibu kwa hasira huku nikimdanganya.
Cha ajabu akacheka sana tena sana. nikashtuka. Akasema:
“Mbona una hasira anko. Kwani kukuuliza jina kuna ubaya? Halafu kama jina lako hupendi watu walijue si unakataa kulitaja tu.”
Hapo nilibaini mambo mawili. Kwanza. Ina maana alijua nimemdanganya jina, pili alijua nimekasirika.
“Unataka kujua jina langu au unataka kujua tabia yangu?” nilimuuliza nikiwa siriasi.
“Jina lako.”
“Frank.”
“Sawa. Mimi naitwa Rehema. Rehema Nyoni.”
Nilishtuka, maana mke wangu anaitwa Rehema Nyoni. Sasa yeye Rehema Nyoni yupi?
“Rehema Nyoni umeolewa?” nilijikuta nikimuuliza hivyo.
“Ndiyo. Mume wangu anaitwa Mussa, nina watoto wawili.”
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu wa kweli unaoitwa Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha.

Note: Only a member of this blog may post a comment.