Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye alisema hayo jana Dar es
Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, kuzungumzia mchakato wa
vikao vya kamati za chama hicho ili kupata wagombea wa ubunge,
uwakilishi na udiwani baada ya mchakato wa kura za maoni kukamilika.
Alisema mchakato huo utaanza kwa kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Agosti 6
na 7 kuchuja na kupitisha wagombea ubunge na uwakilishi. Agosti 8 na 9,
Sekretarieti itakutana ikifuatiwa na Kamati Kuu pia kwa siku mbili
kabla ya Halmashauri Kuu kukutana Agosti 12 na 13 kuteua wagombea ubunge
na uwakilishi.
“Kura za maoni siyo mwisho wa safari, ni hatua ya kwanza ya kuona ni
nani anayekubalika… siyo kibali cha kupeperusha bendera ya CCM, kama
kuna upungufu vikao vitachukua hatua. Kura ya maoni si kigezo… kama
wamecheza rafu au kutumia rushwa, hata kama wameshinda kwa kura nyingi,
ikithibitika wanaweza kuondolewa,” alisema Nape na kuongeza:
“Tutafanya kama ilivyokuwa kwa wagombea urais, kama maadili hayakufuatwa
wanaweza kuondolewa siyo tu wa kwanza, hata wanne, hata kufuta matokeo.
Tutachukua hatua kwenye ubunge, tutachukua hatua kwenye udiwani kwa
wale watakaojihusisha na rushwa. Hawatapata nafasi ya uteuzi kwenye
chama chetu. Hatuna muda wa kuanza kuosha watu na madodoki.”
Alikumbusha jinsi chama hicho kilivyomteua Dk Khamis Kigwangallah
kuwania ubunge wa Nzega alikoteuliwa licha ya kushika nafasi ya tatu
katika kura ya maoni.
Changamoto kura za maoni
Kuhusu changamoto kwenye upigaji kura za maoni ikiwamo vitendo vya
rushwa, Nape alisema kwa takwimu walizonazo, changamoto zilizojitokeza
ni kidogo ikilinganishwa na miaka ya nyuma... “Hii ni kwa sababu
tumeboresha utaratibu tofauti na huko nyuma. Maeneo mengi yamemaliza na
hata yale ambayo yamekuwa na kasoro za hapa na pale tumezitatua.
“…Kura za maoni katika chama chetu zimetoa demokrasia na bila shaka
tumefundisha vyama vingine. Vyama vingi vinatoa wagombea mfukoni, lakini
sisi tunawapeleka kwa wanachama wanapigiwa kura,” alisema Nape.
Vigogo kuanguka
Alisema kuwa kutokana na kukua kwa demokrasia katika chama hicho na
kujenga mfumo mzuri zaidi wa upigaji kura za maoni, hata vigogo
wasiofanya vizuri wameanguka katika kura za maoni.
Kauli hiyo ya Nape imekuja huku kukiwa na ripoti ya baadhi ya mawaziri
na wabunge wanaomaliza muda wao kuanguka katika kura za maoni.
Vigogo kuhama CCM
Alipoulizwa kuhusu kuhama chama hicho kwa waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa na Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga na wanaCCM wengine,
Nape alisema siyo jambo la ajabu na kwamba si wa kwanza na wala
hawatakuwa wa mwisho. “Wapo wanaotoka CCM kwenda vyama vingine na wapo
wanaotoka vyama vingine na kuja CCM. Lakini niseme tu kwamba wapo ambao
wanataka uongozi na wapo ambao wanataka kwenda kuongoza watu:
“Anayetaka kuongoza watu ni mvumilivu, mtulivu na hufuata taratibu.
Lakini wapo ambao lengo siyo kwenda kuongoza watu, lengo ni masilahi
binafsi. Wakikosa uongozi huonyesha tabia zao waziwazi.”


Note: Only a member of this blog may post a comment.