Majeruhi akiwa hospitali.
Na Igenga Mtatiro, MaraHofu kubwa imetanda kwa wakazi wa Wilaya ya Tarime na vitongoji vyake mkoani hapa, baada ya kuibuka kwa mtu aliyepachikwa jina la Kenonke III (kwa lugha ya Kikurya), likiwa na maana ya hiki ni nini, asiyejulikana sura anayedaiwa kuua watu sita na kuwajeruhi wengine akitumia bunduki aina ya SMG.
Katika matukio mawili ya hivi karibuni, mtu huyo maarufu kwa jina la mdunguaji alidaiwa kuhusika na mauaji ya watu hao wakiwamo wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyamongo, Tarime, mmoja wa kidato cha tatu na mwingine cha nne walipokuwa wakitokea shuleni majira ya jioni.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa, mbali na wanafunzi hao, watu wengine waliuawa karibu na Shule ya Msingi ya Nyansangero katika Kijiji cha Komarera Kata ya Nyamwaga wakiwa kwenye bodaboda majira ya saa 2:00 usiku.
Kamanda huyo aliwataja waliouawa kuwa ni pamoja na Marwa Muniko Chagire (20), mkazi wa Kijiji cha Nyamwaga na Gemahe Gichogo (28), mkazi wa Kijiji cha Nyamombasa ambao walipigwa risasi tumboni na vifuani huku Mwita Nyambaswa (19), mkazi wa Kijiji cha Mangucha akimiminiwa risasi pajani na kupoteza fahamu.
Kamanda Mambosasa alisema majeruhi huyo alikimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Tarime kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Musoma kisha Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
Siku chache baadaye wanafunzi wengine wa Shule ya Sekondari ya Nyamongo, Benjamin Winza Jonathan (19) na Mwita Maswi Munanka (23) walipigwa risasi na kufariki dunia papo hapo.
Kamanda Mambosasa aliliambia gazeti hili kuwa jeshi hilo linachunguza na litamkamata mtu huyo hivyo wananchi waondoe hofu.
Mwaka 2013, kuliibuka mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Charles Range Kichune maarufu Kenonke II ambaye alikuwa mkazi wa Kijiji cha Kenyamanyori aliyewaua watu takriban nane na kuwajeruhi wengine kadhaa katika matukio tofauti kabla ya kukamatwa na kufariki dunia akiwa hajafikishwa mahakamani.

Note: Only a member of this blog may post a comment.