Serikali imeshauriwa kununua helikopta
(Chopa) katika kila mkoa kwa ajili ya kufanya shughuli za zimamoto
badala ya kutumia magari ambayo hayafiki kwa wakati katika maeneo ya
matukio kutokana na msongamano wa magari barabarani.
Ushauri huo ulitolewa jana bungeni na Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Muhammad Ibrahim Sanya, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji
kwanini serikali isiwe na utaratibu wa kununua Chopa kwa ajili ya
kuwezesha vikosi vya zimamoto kutokana na miundombinu ya sasa kuwa
mibaya ambayo pia inasababisha magari ya zimamoto kutofika katika maeneo
ya matukio kwa wakati.
“Tumekuwa
tukishuhudia mara kadhaa moto unapotokea magari ya zimamoto yanashindwa
kufika kwa wakati na hiyo ni kutokana na miundombinu kuwa mibovu. Ni
kwanini serikali isione umuhimu wa kununua Chopa ili zitumike kuzima
moto kuokoa maisha na mali za watu?,” alihoji.
Akijibu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alisema wanakubaliana na ushauri huo na kwamba fedha zitakapopatikana watanunua Chopa hizo na kuziweka katika miji mikubwa.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Fakharia Shomari Khamis
(CCM), alisema wananchi wengi hawajui kuwa Kikosi cha Zimamoto ndicho
chenye wajibu wa kuzima moto na badala ya yake hukimbilia polisi hivyo
kukosa msaada wa haraka kuzima moto.
Aliitaka serikali kutoa elimu kwa wananchi ili matukio ya moto yanapotokea watoe taarifa haraka kwenye vikosi hivyo.
Akijibu, Silima alisema Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji ndicho chenye wajibu na dhamana ya kupewa taarifa za ajali na majanga.
Alisema katika kuhakikisha wananchi
wanafahamu juu ya utoaji wa taarifa za ajali na majanga, kikosi hicho
kinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya
habari.


Note: Only a member of this blog may post a comment.