Mawakala wanaoandikisha vitambulisho vya wapigakura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR), katika Kituo cha Shule ya Msingi Umoja, wamegoma kuendelea na uandikishaji kwa madai ya kutolipwa posho.
Akizungumza kwa niaba ya mawakala wenzake katika manispaa ya Kinondoni, Yusufu Msigiti alisema mkataba wao uliisha jana, lakini walipewa malipo ya siku sita badala ya kumi.
Alisema hata walipofuatilia waliambiwa wanapaswa kulipwa na manispaa au Serikali ya kata.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mabibo, Paul Ngunga
alidai kuwa alikaa kikao na mawakala hao akawaeleza kuwa katika
manispaa hiyo, fedha iliyotoka ni ya siku sita tu, hivyo waendelee kuwa
na subira.
“Sehemu
nyingine mawakala wanaendelea na kazi, hawa ndiyo hawajaelewa,
wamegoma…. nimeshaleta mawakala wengine na wanaendelea na kazi ya
kuandikisha wananchi,” alieleza Ngunga. Hata hivyo, Msigiti alisema:
“Hatujawahi kulipwa na watu hao, lakini tunashangaa mtendaji wa kata
anatuambia tuende huko, fedha yenyewe wanayotulipa ni ndogo tunafanya
kazi ngumu kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni.”
Msigiti alisema mtendaji huyo aliwajibu
vibaya baada ya kumhoji kuhusu posho zao za siku nne ambazo hawajalipwa
badala yake aliwaambia anayetaka kazi aendele na asiyetaka aache.
Mawakala hao wamemtupia lawama mtendaji huyo kwa majibu yake ilihali wana malalamiko ya msingi.
Walisema hakukuwa na haja kwa mtendaji huyo kuita polisi kwa lengo la kuwazuia mawakala hao kudai haki yao.
Wakala Peter Mnyika alisema polisi
walivyofika eneo hilo walimpiga mwandishi wa habari aliyekuwa eneo hilo
na kumzuia kukusanya taarifa zake.
“Alikuwa
amevaa kitambulisho na alijitambulisha baada ya kuona vurugu zinazidi
lakini askari mmoja wa kiume alimkunja mwandishi huyo na baada ya kuona
waandishi wenzake wamefika na kamera alikimbilia ofisi ya mwalimu mkuu
na hajatoka mpaka sasa,” Mnyika.
Mwandishi aliyepigwa ambaye hakutaka
kutaja jina lake alisema askari ndiyo wamekuwa wa kwanza kumzuia kufanya
kazi yake badala ya kumpa ushirikiano.
Yusufu Kileme alikiri mtendaji wa kata kutumia lugha mbaya wakati mawakala wakidai haki yao. Pia, alisema askari wanaofika eneo hilo wanapaswa kuangalia anafanya fujo ili wazuie, na siyo kuwa chanzo cha vurugu.
Mwenyekiti wa kata hiyo, Saimoni Ramo
alisema askari walipofika aliwasihi wasitumie nguvu kwa sababu
malalamiko ya vijana hao ni ya msingi.
Note: Only a member of this blog may post a comment.