Kwenye baadhi ya maeneo kazi hiyo iliahirishwa hadi leo kutokana na
vifaa kuchelewa na pia tatizo la kugundulika kwa shahada ambazo
zimeshapigwa kura zikiwa ndani ya maboksi.
Lakini matukio yaliyotawala kura za maoni ni makada kukamatwa kwa tuhuma
za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha au kuchapisha
karatasi bandia za kupigia kura.
Dar es Salaam
Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Takukuru inawashikilia wagombea
sita kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe ili wachaguliwe kwenye kura
za maoni.
Makamu mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Denis Manumbu aliwataja
waliokamatwa kuwa ni katibu wa kata ya Kibamba, Denisi Kalela, katibu wa
itikadi, Babu Kimanyo, diwani wa viti maalumu wa Goba, Rehema Luhanja,
Wengine ni mwenyekiti kata ya Goba, Pili Mustafa, mgombea udiwani,
Msigani Mwasha na Eliasi Nawera ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kawe.
Alisema kuwa Kalela, na Kimanyo walikamatwa juzi saa 4:00 usiku maeneo
ya Kibamba CCM, huku Mustafa na Luhanja wakikamatwa maeneo ya Goba Kati
na Kawe.
“Walikamatwa wakiwa wanatoa rushwa na wengine walikamatwa wakiwa na
kiasi cha pesa ambazo bado walikuwa wanazigawa huku wengine
wakiwashawishi wajumbe kupokea rushwa,” alieleza Manumbu.
Manumbu alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi ofisi yao inafanya kazi saa 24 ikipokea taarifa zote zinazohusu rushwa.
Kondoa
Lakini hali ilikuwa mbaya wilayani Kondoa, Dodoma ambako CCM ililazimika
kuchoma moto makasha sita ya kupigia kura baada ya kubainika kuwa
baadhi ya wanachama walitumia kadi ya CCM pekee bila ya kitambulisho cha
kupigia kura.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Shaaban Kissu, mwenyekiti wa CCM wa wilaya,
Othman Gora na kamanda wa polisi wa wilaya, Nyantora walikubaliana
kuchomwa moto baada ya kubaini tatizo hilo.
Hatua hiyo, inatokana na wanachama kuanzisha zogo kuwa vitambulisho vya
kura havikutumika kabla ya uamuzi huo kufikiwa. Tayari zaidi ya
wanachama 200 walikuwa wamepiga kura hizo.
Maboksi hayo yalichomwa mbele ya kituo cha kupigia kura cha Ubembeni na
kushuhudiwa na wananchi, wananchama wa CCM, polisi na uongozi wa CCM.
Baada ya kuyachoma, Kissu alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya dosari hiyo na kwamba utarudiwa leo.
Baadaye kamanda wa polisi wa wilaya aliamrisha watu wote kutawanyika eneo hilo hadi leo.
Awali kulitokea vurugu baada ya baadhi ya wanachama kunyakua sanduku
lililokuwa na kura na kutaka kukimbia nalo kwa tuhuma kuwa mawakala
hawakuwa wakitenda haki kwa wapiga kura
Mbeya
Kashfa ya matumizi ya rushwa pia ilijitokeza mkoani Mbeya ambako mgombea
udiwani mmoja kulalamikiwa kwa madai ya kuwakodisha wanafunzi wampigie
kura kwa malipo ya Sh2,000 kwa kila mmoja.
Mgombea huyo wa udiwani wa Kata ya Mbalizi Road analalamikiwa pia
alikwenda kwenye kilabu za pombe kuwatafuta watu wanaotaka kumpigia kura
ili awanunulie kinywaji.
Miongoni mwa walalamikaji ni Ally Salum na Aziza Mbika wa eneo la
Sabasaba ambao walisema walimwona mgombea huyo akitoa fedha na pombe kwa
vijana mbalimbali .
Msimamizi wa uchaguzi wa Kituo cha Meta, Ndoni Mwakalukwa alikiri
kupokea malalamiko ingawa hakushuhudia utoaji wa fedha hizo na kwamba
atayazungumza baada ya kumaliza kazi ya upigaji kura.
Vituo vingine, vikiwamo vya Kata za Ruanda na Sinde, vilikosa wanachama
wa kupiga kura na badala yake walifika mmoja mmoja kila baada ya saa
kupita.
Wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo walikuwa na kazi ngumu ya kuwaita
watu waliokuwa wakipita wakiwaomba wakapige kura kama ni wanachama wa
CCM.
“Tatizo ni kwamba vituo vya kupigia kura havijawekewa alama yoyote,
hivyo wanachama wengi hawajui,’’ alisema msimamizi wa kituo cha Soweto,
Ambakisye Kitunga.
Lindi
Rushwa pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Mchinga (CCM) ambako mbunge wa
viti maalumu, Fatuma Mikidadi alikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutoa
rushwa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo waliomkamata kwa tuhuma za
hongo.
Habari zinasema kuwa mgombea huyo alikutwa na wafanyakazi wa Takukuru akitoa rushwa kwa wanachama wa Kata ya Mchinga.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mikidadi alikasirika akisema: “Uongo, uongo, huu ni uzushi kabisa.”
Alipoulizwa kwa nini anafikiri wamemsingizia, alisema: “sijui hawa
wanasingizia singizia tu, uongo.” Hata hivyo, kamanda wa Takukuru wa
mkoa wa Lindi, Steven Chami alisema Fatuma alikamatwa saa 5:00 usiku
Kata ya Mchinga akigawa fedha kwa wanachama.
Chami alisema akiwa ofisi za Takukuru baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo
alitoa tena Sh780,000 kwa ajili ya kuwahonga maofisa hao ili
wasiendelee na suala hilo.
Alisema kutokana na kitendo hicho, Takukuru itamfikisha mahakamani muda
wowote baada ya mwanasheria kutafsiri na kubainisha tuhuma zake.
Wakati huohuo, kamanda huyo alisema mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi
Mjini, Mohamedi Utali alishikiliwa kwa muda wa saa kadha kwa mahojiano
na Takukuru baada ya kukutwa na Sh4milioni saa 8:30 usiku akiwa Kata ya
Mbanja.
Chami alisema kukamatwa kwa mgombea huyo kulitokana na ushirikiano baina ya wananchi na taasisi hiyo.
Shinyanga
Mjini Shinyanga, katibu wa Kata ya Mjini Shinyanga, Ramadhani Majani
amenusurika kipigo baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa
ofisini kwake na mmoja wa wagombea udiwani na ubunge katika Jimbo la
Shinyanga Mjini.
Mashuhuda wa tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari jana kwamba
Majani alikutwa na kadhia hiyo baada ya watu waliotilia shaka nyendo
zake kwa kitendo chake cha kuongozana na mmoja wa wagombea nyakati za
usiku kuingia ofisini na hivyo kuhisi kuna jambo lisilokuwa la kawaida
walilopanga kufanya.
Walisema waliamua kuwapigia simu wagombea wengine waliokwenda ofisi hizo
na kumkuta mgombea mmoja (jina limehifadhiwa) akiwa anaongea naye, hata
hivyo walishituka ghafla baada ya kuona kundi la wana-CCM wakijongea
ofisini hapo.
“Sisi tulipigiwa simu usiku saa 4:45 na baadhi ya watu wanaoishi jirani
na ofisi yetu ya kata kwamba wamemuona katibu kata wetu akiwa na mgombea
udiwani pamoja na wapambe wake. Walidai inavyoelekea walikuwa wakipanga
mikakati mibovu ya kutaka kuiba kura,” alisema Rashidi Abdalah.
“Taarifa hizo zilitushangaza sana. tuliamua kuchukua gari na kwenda
katika eneo la ofisi na kweli tulimkuta katibu kata akiwa na mgombea
(anamtaja jina) wakiwa nje ya ofisi za CCM wakitaka kuingia ndani,
ghafla walipotuona mgombea na wapambe wake walikimbia na katibu kata
aliingia ofisini na kuufunga mlango,” alieleza aliongeza.
Abdalah alidai kitendo cha Majani kukimbilia ofisini kilisababisha
baadhi ya watu kushikwa na hasira na kutishia kuvunja mlango ili kumtoa
nje na kumshushia kipigo, lakini mgombea
mwingine alimsihi ajisalimishe na kufanikiwa kutuliza ghasia.
Majani alikiri kutaka kupigwa na kundi la wana-CCM na kwamba ni kweli
muda huo wa usiku alikuwa ofisini akifanya kazi ya kugonga muhuri kwenye
karatasi za kupigia kura japo hakuweza kufafanua kitendo cha mmoja wa
wagombea kuwa katika maeneo hayo nyakati hizo za usiku.
“Nilikuwa naendelea na kazi zangu lakini baadaye nilishangaa watu
wanakuja na fimbo wakidai niko na mgombea ilibidi nijifungie ofisini
kwangu,” alisema Majani.
Handeni
Hali ya sintofahamu ilitanda kwenye tawi la Bomani, Kata ya Vibaoni
wakati zaidi ya wanachama 60 walipogoma kupigia kura wagombea udiwani
kwa maelezo kuwa hawawafahamu kwa kuwa hawakufika eneo hilo kujinadi na
badala yake kuamua kupiga kura ya wagombea ubunge.
Wakizungumza jana wakati wa kuwasubiri wagombea, wanachama hao walisema
kuwa walikutana kuanzia saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kuwasubiri, lakini
hawakutokea hadi saa 12:00 jioni, kitu ambacho walidai kuwa ni dharau.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani, John Mohamed alisema kuwa walikubaliana
kukutana na madiwani hao kwa mara ya kwanza, lakini akidi ya wanachama
haikutimia ikawabidi kuahirisha kikao hicho hadi jana lakini kitu cha
ajabu wagombea hao hawakutokea hadi jioni.
Arusha
Sakata la karatasi bandia za kupigia kura pia liliibuka mkoani Arusha,
ambako viongozi wawili wa CCM walikamatwa kwa tuhuma hizo. Waliokamatwa
ni katibu wa Kata ya Mjini Kati, Ally Meku na mwenyekiti wa Mtaa wa
Bondeni, Yakub Shaban.
Katibu wa Wilaya ya Arusha, Feruz Bano alisema: “Ni kweli wamekamatwa,
lakini tunafuatilia kujua kosa lao kwa kuwa hawana ofisi, hivyo walikuwa
wanapeleka karatasi hizo kwenye chumba cha kupigia kura kidogo kidogo,”
alisema.
Dodoma
Rafu iligubika uchaguzi huo mkoani Dodoma ambako baadhi ya wanachama
walikamatwa na shahada bandia, huku vurugu zikiripotiwa maeneo kadhaa.
Waliokamatwa na tuhuma kuwa walikuwa na shahada bandia ni katibu wa
vijana Tawi la Chang’ombe, Nasra Salum akiwa na shahada 20 za kupigia
kura, 20 za udiwani, Bakari Fundikira (za ubunge), na David Malolle.
Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma hizo ni Faisi Mussa ambaye CCM imeeleza alikutwa na shahada 15 bandia.
Aidha, baadhi ya kata zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana sababu
mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na karatasi za kupigia kura kuwa
na makosa. Miongoni mwa kata zilizoshindwa kufanya uchaguzi huo ni
Tambukareli na Kilimani mjini Dodoma.
Katibu wa CCM wa mkoa, Albert Mgumba alisema kata ambazo hazijafanya
uchaguzi, kazi hiyo itafanyika leo kabla ya saa 4:00 asubuhi. Kuhusu
makada waliokamatwa, katibu huyo alisema jambo hilo waulizwe makatibu wa
wilaya kwa kuwa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, vurugu zimetokea katika tawi la Mji Mpya lililoko
Kata ya Uhuru kutokana na baadhi ya wanachama kudai kuna mamluki
wameingia kupiga kura.
“Asubuhi walikuja watu kutoka Tawi la Uhuru wakidai kuwa kuna mamluki
wanataka kupiga kura kwenye tawi letu, lakini baada ya viongozi kufika
tulirekebisha na zoezi likaendelea kwa amani na utulivu,” alisema
msimamizi wa kituo hicho, Mariam Jumbe.
Bukoba
Hali ilikuwa tofauti mkoa Kagera ambako uchaguzi huo majina ya wanachama
waliofariki dunia yalikuwapo kwenye orodha ya wapiga kura Jimbo la
Nkenge huku kukiwa na hofu ya kuanguka kwa vigogo.
Hali hiyo ilitokea katika vituo vya Mutemba na Igayaza. Hata hivyo,
katibu wa CCM wa Wilaya ya Missenyi, Mwajuma Mboha alisema kujulikana
kwa majina hayo, ni matunda ya uwepo wa mawakala katika uchaguzi huo.
Pia kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya watu
waliofika kupigakura. Katika kata hiyo ya Nsunga kulikuwa na watu saba
waliolalamikia kutoorodheshwa.
Mtwara
Kukosekana kwa majina katika orodha ya wapigakura pia ilijitokeza kwenye Manispaa ya Mtwara Mindindani.
Wakiongea na Mwananchi, Shangani Aisha Ismail na Salima Nassoro wa Tawi
la Vigaeni walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa CCM kuwapa
kadi za chama bila kuweka majina yao katika daftari la wapigakura.
“Sisi tumepewa kadi tunazo mikononi hatujui kama nyingine zimesajiliwa
au la. Nyingine tumezilipia na majina yetu hayapo. Kuna kadi nyingine za
mwaka 2000 hadi mwaka 1950 zipo na majina yao yapo na sisi majina yetu
hayapo kuna nini hapa?” alihoji Aisha
Katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya, Mohamed Watanga alikiri kuwapo na tatizo hilo, akieleza kuwa wanalitafutia ufumbuzi.
Njombe
Pia mkoani Njombe, wanachama walishindwa kupigakura kutokana na kadi zao
za uanachama kuonekana kuwa zilikatwa baada ya Julai 15, siku ambayo
CCM ilifunga kazi ya kuandikisha wanachama wapya.
Msimamizi wa uchaguzi wa kituo cha Mpechi, Sarah Nyandoa alisema licha
ya uchaguzi kufanyika kwa amani, alikiri kuwapo kwa wanachama waliokuwa
na kazi walizopata baada ya Julai 15.
“Ni kweli kuna baadhi ya watu wanakuja na kadi zao zilizochukuliwa baada
ya Julai 18, lakini tumewarudisha baada ya kuwaelimisha wameridhika,”
alisema Nyadoa.
Pwani
Mchakato kura za maoni umeingia dosari katika vituo kadhaa baada ya
baadhi ya wanachama kukatwa majina yao kwenye daftari la orodha ya
wanachama wa chama hicho.
Mbali ya kuwepo majina yaliyokatwa, pia baadhi ya wanachama walikutwa
wakipiga kura kwa kutumia stakabadhi ya malipo ya wanachama maarufu
badala ya kutumia kadi ya uanachama wa CCM.
Kasoro hizo zilisababisha vurugu kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura
mjini Kibaha na kumlazimu mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid
Bundala kusitisha uchaguzi huo kwenye vituo kadhaa vilivyokua na kasoro.
Bundala alisema jana mchana kuwa vituo vilivyofutiwa kufanya uchaguzi ni
Morning Star na Machinjioni vilivyoko Kata ya Tangini mjini Kibaha.
Uchaguzi huo utarudiwa leo.
Alipoulizwa sababu za kuwepo tofauti ya idadi ya majina yaliyomo kwenye
daftari la uanachama na idadi ya wenye kadi za chama eneo hilo, alisema
wamebaini kasoro hiyo imesababishwa na baadhi ya mabalozi kutowasajili
kwenye daftari la chama la wapigakura.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachama waliokuwa wakipiga kura
Kibaha Mjini wamelalamikia kuwepo rafu katika mchakato wa upigaji kura
wakisema baadhi ya matawi yaliweka orodha kubwa ya wanachama
wanaoruhusiwa kupiga kura ikilinganishwa na idadi ya awali iliyobandikwa
kwenye kuta za ofisi za matawi yao.
Tarime
Mjini Tarime mkoa wa Mara, uchaguzi ulilazimika kuahirishwa hadi leo
baada ya kukamatwa kwa karatasi bandia za kupigia zilizokuwa
zimeshawekewa alama ya ndiyo kwa wagombea wa ubunge Jimbo la Tarime, na
Tarime Mjini.
habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa karatasi hizo zinazoendelea
kukusanywa, zilitengenezwa na mmoja wa viongozi wa wilaya, Bernard
Nyerembe ambaye amekamatwa na kufikishwa Takukuru kwa mahojiano zaidi.
Habari hizo zinasema kuwa karatasi hizo zilikuwa zichanganywe na karatasi halali baada ya wanachama kupiga kura za maoni.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Rashid Bogomba alithibitisha kukamatwa kwa karatasi hizo jana asubuhi.
Alisema kwa Jimbo la Tarime, kura hizo zimekamatiwa katika vijiji vya
Nyamwaga, Masanga na Nyamongo na kwa Jimbo la Tarime Mjini zimekamatwa
Mtaa wa Bomani, Magena na Romori.
Bogomba alisema kutokana na kukamatwa kwa karatasi hizo, uchaguzi umeahirishwa.
Kamanda wa polisi wa Tarime/Rorya, Benadict Mambosasa pia alithibitisha
kukamatwa kwa Nyerembe na kwamba amepelekwa Takukuru kuhojiwa. Alisema
Nyerembe alikamatwa akiwa ofisi ya CCM ya wilaya baada ya wanachama
kumtuhumu kuwa alikuwa na karatasi zilizokwishapigwa kura kwa ajili ya
wagombea wawili wa majimbo hayo.
Mwananchi ilipomtafuta Nyambari Nyangwine anayetetea ubunge wa Tarime,
na Waziri Gaudensia Kabaka (Tarime Mjini) wote wwalikanusha kuhusika na
kudai hizo ni njama zilizopikwa dhidi yao.
Makada wengine wanaowania ubunge wa Tarime ni Christopher Kangoye ambaye
ni mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nyambari Nyangwine (mbunge), Pius Marwa,
John Gimunta, Maseke Muhono, Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles
Machage.
Kwa jimbo jipya la Tarime Mjini wanaogombea ni Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudensia Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani Machango,
Ditu Manko na Brito Burure.
*Imeandikwa na Dinna Maningo, Suzy Butondo, Julieth Ngarabali,
Phinias Bashaya, Brandy Nelson, Hawa Mathias, Justa Mussa, Godfrey
Kahango, Rajabu Athumani, Mwanja Ibadi, Mussa Juma, Sharon Sauwa, Mary
Sanyiwa, Shaban Lupimo, Beatrice Moses na Emma Kalalu.
Note: Only a member of this blog may post a comment.