Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya nchi, Lawrence Masha amemkwepa hasimu wake kisiasa, Ezekia Wenje(Pichani)
katika Jimbo la Nyamagana, Mwanza na kwenda kugombea ubunge Sengerema
ambako atavaana na mbunge anayemaliza muda wake, William Ngeleja.
Katika uchaguzi uliopita mwaka 2010,
Masha aligombea kipindi cha pili katika Jimbo la Nyamagana (CCM), katika
mpambano uliokuwa na ushindani mkali na kuangushwa na Wenje wa Chadema.
Awali, kabla ya uchaguzi huo, Masha
akiwa waziri mwenye dhamana na mambo ya ndani, alimwekea pingamizi Wenje
akidai hakuwa raia, lakini hoja hiyo haikumzuia mshindani wake, badala
yake ilimwongezea kura za huruma hadi akaibuka mshindi.
Safari hii Masha amepima maji na kuamua kumvaa waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Ngeleja ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa wanaCCM 38 walioomba kuwania urais, lakini akaondolewa katika hatua za awali.
Alipoulizwa jana, Masha alisema
amechukua fomu Sengerema kwa sababu ni nyumbani kwao, ndipo alikozaliwa
na kukulia, hivyo ameamua kushirikiana nao kusukuma gurudumu la
maendeleo.
“Nyamagana
pia ni nyumbani, hivyo tutaendelea kushirikiana ili kuleta maendeleo
kwa kila jimbo. Sijafanya maridhiano yoyote ya kuachiana jimbo, lakini
natumia haki yangu ya kugombea popote,” alisema.
Hata hivyo, hata katika jimbo la
Sengerema alikoomba kugombea hayuko salama kutokana na nguvu ya upinzani
iliyopo kupitia Chadema ambacho nguvu yake ilidhihirika katika Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa Desemba mwaka jana pale ilipochukua viti vyote
katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Sengerema na maeneo mengine ya vijijini.
Mbali na Masha na Ngeleja, wengine waliojitokeza katika jimbo hilo kupitia CCM ni Anna
Shija, George Rweyemamu, Philemon Tano, Dk Omari Sukari, Dk Angelina
Samike, Jumanne Mabawa, Mussa Malima, Baraka Malebele, Joshua Shimiyu na
Zablon Bugingo.


Note: Only a member of this blog may post a comment.