KWENU wasanii mliothubutu kujipambanua kwa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa. Vipi mko poa? Poleni kwa kuyeyuka kwa ‘safari ya matumaini.’
Leo nimewakumbuka kupitia barua. Nina jambo nataka kuwaambia. Si lingine bali ni suala la mchujo wa wagombea wa urais wa CCM uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma.
Kifupi najua mpo wengi mliokuwa mnamuunga mkono aliyekuwa mtangaza nia, Edward Lowassa.
Sina haja ya kuwataja majina kwani mpo wengi lakini nataka kuwaambia tu kuwa hamisheni nguvu yenu kwa mgombea aliyepitishwa na chama hicho, John Pombe Joseph Magufuli.
Najua mna maumivu, hasira ya kukosa ushindi na baadhi yenu tayari mmeshaanza kuonesha chuki za wazi kwenye mitandao ya kijamii. Badilikeni. Mnapaswa kuwa kitu kimoja kwa sasa.
Taratibu na kanuni za chama hicho mnazijua. Mnakuwa na kambi pale tu mnapoanza mchakato wa kutangaza nia. Watangaza nia walikuwa 42, mwisho wa siku lazima apatikane mmoja. Vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu vimeshatenda kazi yake, tena nzuri tu.
Wameangalia sifa na vigezo na kudhihirisha haki imetendeka, mmeona jinsi Mkutano Mkuu ulivyompigia kura nyingi Magufuli. Kura 2,104 ambazo ni sawa na asilimia 87.1 ni kielelezo cha kuonesha kwamba alistahili, hamna budi kumuunga mkono.
Kama mlikuwa mnamuunga mkono Lowassa, mlikuwa mnakiunga mkono Chama cha Mapinduzi. Taratibu za kichama zilimuengua kwa vigezo, hakuna haja ya kuanza kutafuta mabaya ya Magufuli eti mkifikiri mtamkomoa, mtajikomoa wenyewe.
Chuki hazijengi. Uzuri ni kwamba hata kama hamkiri hadharani lakini moyoni mnatambua kwamba Magufuli ni mpambanaji. Ni mchapakazi ambaye hahitaji nguvu ya ziada kumuelezea mbele ya jamii ya Watanzania kutokana na historia yake.
Amekuwa mstari wa mbele kusimamia sheria. Anajua ‘kupush’ mambo kwa vitendo na hiyo imejidhihirisha katika wizara zote alizopitia. Niwaombe tu kiroho safi, kwa manufaa ya chama, hamishieni nguvu kwa Magufuli na maisha yaendelee.
Ni matumaini yangu mtakuwa mmenisoma, nawatakia utekelezaji mwema.
Wenu katika ujenzi wa taifa,
Note: Only a member of this blog may post a comment.