Mpenzi msomaji baada ya utambulisho juu ya hawa jamaa, wiki iliyopita nilianza kugusia juu ya orodha ya Freemasons.
SASA ENDELEA…
Katika orodha hiyo unakutana na majina kadhaa ya watu mashuhuri kutoka kwenye tasnia tofauti wakiwemo viongozi wa dini kama Swami Vivekananda, askofu mkuu wa zamani wa Canterbury, mchungaji Geoffrey Fisher, wanaharakati kama Jesse Jackson, wafanyabiashara kama Fords, Rothschilds na Rockefellers (humo kuna mwanamuziki wa Marekani, Jay-Z ambaye katika simulizi hii, baadaye matoleo yajayo nitakupa stori yake kamili) na Richard Wagner. Watu kama Mozart, Shakespeare, Rudyard Kipling na Alexander Fleming pia ni kati ya Freemasons maarufu. Hata Neil Armstrong, mwanadamu wa kwanza kutua kwenye mwezi anatajwa kwenye listi hiyo.
Hapa Tanzania ripoti zinaonesha wanachama hai ni zaidi ya 600. Ni kundi la watu wenye imani ya siri ya Freemasons. Inaelezwa kwamba ni watu wa kada mbalimbali wakiwemo maarufu au mastaa. Kuna maelezo yanayodai kuwa wapo viongozi na waliowahi kuwa viongozi wa ngazi za juu kabisa serikalini lakini wenyewe hawajawahi kuzungumza juu ya hilo. Ukiwauliza watakuambia ni habari za mtaani tu. Labda kwa sababu ni suala la siri sana. Kwanza hata wenyewe hawapendi kuulizwa juu ya mambo hayo.
Kwa mujibu wa Kiongozi wa Freemasons katika eneo la Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande maarufu kama Sir Andy Chande ambaye ni Mtanzania, mkazi wa Dar es Salaam, mwenye asili ya Kiasia, licha ya Tanzania kuwa na wanachama hao, kwa sasa idadi ya Freemasons duniani inapungua tofauti na inavyodaiwa na watu wasiyoijua kwamba wanaongezeka kutokana na kuibuka kwa stori nyingi kuhusu wao.
Katika simulizi yake juu ya Freemasons, Sir Andy Chande ambaye kwa sasa amestaafu anasisitiza kuwa si rahisi kumjua mwanachama wa kundi hilo, bali wenyewe ndiyo wanaofahamiana.
Sir Chande anasema ni siri sana na kwamba wenyewe wanakutana katika vikao mbalimbali mara moja kwa mwezi au zaidi. Kiongozi huyo anasema kwamba wanachama wake zaidi ya 600 wakiwemo wafanyabiashara, watumishi serikalini, walimu pamoja na wanataaluma mbalimbali wanaoheshimika sana na kusisitiza kuwa kuna maneno mengi yanayosemwa kuhusu kundi hilo, ambayo siyo ya kweli.
Kwa mujibu wa Chande, duniani kuna watu wazito wengi ambao ni wanachama wa kundi hilo kama majaji wakubwa na hata binamu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza.
Kiongozi huyo anasema masharti ya kujiunga na kundi hilo, ni lazima anayetaka uanachama awe anaamini katika Mungu bila kubagua. Anaweza kuwa Mkristo au Muislam au dini nyingine yoyote.
Chande anasisitiza kuwa anayetaka kujiunga nao ni lazima awe na umri unaozidi miaka 21 na walio chini ya umri huo hawaruhusiwi kujiunga na lazima familia ya anayetaka kujiunga na wanandugu wafahamu kuwa amejiunga na kundi hilo.
Uchunguzi umeonesha kuwa viongozi wengi wakuu wa serikali nchini Tanzania wanafahamu shughuli za Freemasons ambao Chande amekuwa akionekana nao kwenye picha.
Baadhi ya viongozi hao, bila kutaja kama wao ni wanachama ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Marais wastaafu wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa.
Katika kitabu chake kiitwacho Shujaa wa Afrika, Safari kutoka Bukene, Chande anatanguliza shukurani kwa Mkapa na kwamba alifahamiana naye baada ya kumuingiza katika bodi ya Shule ya Shaaban Robert.
Sir Chande anasema anashukuru kutambuliwa na kupewa heshima na vyombo vya kitaifa na kimataifa.
Japokuwa hakuna anayejua wanachokifanya wanachama wa Freemasons lakini inaaminika kuwa viongozi wakuu wa nchi hii wanajua kila kitu.
Usikose kila Jumatano katika mtandao huu huu wa kandiliyetu.com
Note: Only a member of this blog may post a comment.