Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, zengwe hilo linahusu kile kinachodaiwa kuwa ni kuanza kwake mapema kufanya kampeni katika mikutano kadhaa anayoifanya kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini, tangu alipoibuka kidedea katika vikao vya mchujo ndani ya chama hicho tawala, vilivyomalizika hivi karibuni mkoani Dodoma.
“Hii ni kampeni kabisa, tunaangalia uwezekano wa kumshtaki kwa Tume ya Uchaguzi au mahakamani ili haki itendeke, haiwezekani muda wa kufanya kampeni bado yeye anazunguka kujinadi kwa wapiga kura, hii haikubaliki,” alisema kiongozi mmoja kutoka vyama vilivyo katika muungano wa Ukawa, aliyekataa jina lake kuandikwa gazetini, kwa kuwa siyo msemaji wa umoja huo.
Akizungumzia tuhuma hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema siyo kweli kwamba mgombea wao ameanza kampeni mapema, bali kinachofanyika ni utambulisho kwa wanachama wenzake wa CCM, ili wamtambue, kwa kuzingatia kuwa ni mwenyekiti mtarajiwa wa chama hicho tawala.
Alisema ni vigumu kwa mgombea huyo kupita mkoa wowote bila kwenda kwenye ofisi ya chama kwa ajili ya kutambulishwa kabla ya kuanza kwa kampeni baadaye mwezi ujao.
Akiwa mkoani Mwanza wiki iliyopita, Dk. Magufuli alisema yupo njiani kwenda nyumbani kwao Chato na kukanusha juu ya kufanya kampeni, kwani kinachofanyika ni utambulisho na salamu tu.
Note: Only a member of this blog may post a comment.