Tuesday, July 21, 2015

Anonymous

KILICHOMKUTA BINTI HUYU MWANAFUNZI TOKA MOROGORO INASIKITISHA SANA! SHUKA NAYO HAPA TAFADHALI....

Na Makongoro Oging’ 
“Nipo katika hali mbaya, nahitaji msaada wa haraka ili niweze kupona nikajiunge na wanafunzi wenzangu kwa ajili ya maandali ya mtihani wa darasa la saba, bila kupata huo msaada wa kushughulikia ugonjwa wangu huu mapema kuna kila dalili ya kutofanya mtihani huo, ugonjwa umenikatisha ndoto zangu.”

Hicho ni kilio cha mwanafunzi wa darasa la saba, Veronica Peter (13) anayesoma katika Shule ya Msingi Lumbija, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa na Mishipa (MOI).

Akisimulia zaidi mateso yake ya ugonjwa huo alioanza kuugua muda mfupi alisema:

“Ni miezi mitatu sasa tangu ugonjwa huu unianze lakini kwangu naona kama miaka mingi, maumivu ninayoyapata ni makali kuliko kawaida, madaktari wa Mkoa wa Morogoro wamejitahidi ikashindikana hali iliyosababisha niletwe hapa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

CHANZO CHA UGONJWA
“Ugonjwa huu umenianza Mei mwaka huu, nilisikia maumivu kwa mbali katika goti, baadaye nikawa natembea kwa kuchechemea, nilikuwa nikienda shule hivyo hivyo, maumivu yakawa yanazidi, ilibidi mama anipeleke Hospitali ya Wilaya Kilosa.

“Wazazi wangu ni watu wenye kipato cha chini kabisa, wamekuwa wakitegemea kilimo kupata fedha, walihangaika sana nami kwani Hospitali ya Kilosa walishindwa, walifikiri kwamba ni jipu, walilipasua lakini hapakutoa usaha bali ilitoka damu.

MADAKTARI NAO
“Madaktari waliwaeleza wazazi nipelekwe hospitali ya mkoa wetu wa Morogoro, hata hivyo, hawakuwa na fedha kwa ajili ya nauli wala matibabu hali iliyowafanya madaktari wa Kilosa waweze kutoa gari hadi hospitali ya mkoa ambapo nililazwa.

“Madaktari Hospitali ya Morogoro walinifanyia vipimo lakini hawakupata ugonjwa, walinichoma sindano kwa ajili ya kutuliza maumivu kisha wakawaeleza wazazi wangu kuwa nipelekwe Muhimbili.

KULETWA MUHIMBILI
“Hali ya kifedha ilikuwa mbaya kwao waliamua turudi nyumbani wakatumie mitishamba kunitibia, hata hivyo, daktari mmoja alisikia baba akisema hivyo ndipo uongozi wa hospitali ulitoa gari na kunileta hapa Muhimbili.

“Hapa Muhimbili nimefika Julai 8, mwaka huu nikiwa katika hali mbaya kwani mguu ulizidi kuvimba huku nikipata maumivu makali sana na nimekuwa sipati usingizi kutokana na maumivu, kwa sasa madaktari wamekuja kuniangalia na kunifanyia vipimo.

“Ninasubiri majibu, sijajua hali itakuaje, nawashukuru sana madaktari na wauguzi wa wodi hii namba mbili ya Mwaisela kwa kuwa karibu nami muda wote.

“Nimeletwa na shangazi yangu, Adelina Jacob hapa hospitalini kutokana na wazazi wangu kuwa wagonjwa kwa wakati mmoja, nina hali mbaya naomba msaada kwenu,” alisema huku akilengwalengwa na machozi.
Yeyote aliyeguswa na kilio cha mtoto huyu anaweza kumsaidia kwa kutumia namba ya simu ya afisa wa ustawi wa jamii ambayo ni 0715 316302.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.