Kikongwe Yohana Msumari
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 80, ameuawa kikatili kwa
kutenganishwa mwili na kichwa na kisha wauaji hao kukihifadhi kichwa
hicho kwenye mfuko wa plastiki chini ya mwembe.
Hata hivyo mtu anayesadikiwa kufanya
mauaji hayo, alisakwa na wananchi wenye hasira na kisha kukamatwa na
kuonesha mwili wa marehemu huyo na yeye kupigwa na hatimaye kuuawa pia.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea
juzi, katika kijiji cha Mamboleo, Kata ya Bwembwera wilayani Muheza
mkoani Tanga, ambapo kikongwe huyo aliondoka na kijana ambaye naye
hakutambulika jina lake mwenye umri wa kati ya miaka 35-40 wa kabila la
Kinyaturu, ambaye alikuwa mfanyakazi za vibarua kwenye mashamba ya watu.
Akisimulia tukio hilo, Katibu Kata wa
Chama Cha Mapinduzi kwenye Kata ya Bwembwera, Achi Semhando alisema
tukio hilo la kusikitisha lilitokea kwenye kata yao na kwamba polisi
walifika baada ya kupewa taarifa hizo na kuchukia maiti.
“Kwa
kweli ni tukio la kusikitisha, huyu mzee aliondoka na huyo kijana na
kwenda kumuonesha sehemu ya kufyeka shambani kwake, ila hadi jioni huyu
mzee hakurudi na ndipo wananchi waliingiwa na wasiwasi na kuamua
kumtafuta huyo kijana aliyeondoka naye,” Semhando.
Kijana huyo alipatikana na wananchi
walimtaka aseme mzee huyo alipo na ndipo aliwapeleka hadi shambani na
kuona maiti ya mzee huyo na ndipo walianza kumpiga hadi umauti wake na
kisha kutoa taarifa polisi.
Hata hivyo maiti ya mzee huyo haikuwa na
kichwa na polisi walizichukua maiti zote mbili na kwamba ilipofika jana
asubuhi, watoto waliokuwa wakiokota maembe kwenye miti waliona mfuko
umefungwa na walipouchunguza waliona kichwa na kutoa taarifa kijijini.


Note: Only a member of this blog may post a comment.