Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa kumsomea maelezo ya awali Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya matusi na kushindwa kuhifadhi silaha.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya
washitakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini iliahirishwa kwa kuwa
Hakimu Mkazi Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo
mahakamani.
Hakimu Mkazi, Thomas Simba
aliahirisha kesi hiyo hiyo Julai 20, mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa
hao kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Dyansobera.
Mbali na Gwajima washitakiwa wengine, ni Mlinzi wake, George Mzava, Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria.
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima
anadaiwa kati ya Machi16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika
Packers Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi
ya Askofu wa Kanisa Katoliki Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akimueleza Askofu kwamba ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa amani.
Katika kesi nyingine namba 84 , Gwajima
anakabiliwa na mashitaka ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi jambo
ambalo ni kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kati ya Machi 27 na 29, mwaka
huu, ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha
aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi 3 za pisto na risasi 17 za
shotgun.
Katika mashitaka mengine yanayowakabili
washitakiwa wengine, inadaiwa Machi 29, mwaka huu katika Hospitali ya
TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa
kutoka mamlaka husika.

Note: Only a member of this blog may post a comment.