Charles Mkwasa kocha wa muda wa Taifa Stars
Nicodemus Jonas na Saphyna MlawaDar es SalaamRAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, jana alimtangaza rasmi Charles Mkwasa kuwa kocha wa muda wa Taifa Stars akichukua nafasi ya Mart Nooij, aliyesitishiwa ajira.
Malinzi aliliambia Championi Jumatano kuwa, Mkwasa licha ya kuichukua timu kwa muda, atapewa kila kitu alichokuwa akipata Nooij raia wa Uholanzi.
Kocha Charles Mkwasa.
Miongoni mwa vitu hivyo ni, nyumba maeneo ya Masaki, gari, mshahara
pamoja na posho. Malinzi alisema: “Lakini hii itategemea na majibu ya
serikali kwani tumewatumia barua ya kuomba hivyo.”TFF imemalizana na Nooij na jana alitarajiwa kupewa stahiki zake zote kwa kuvunjiwa mkataba ikiwemo fedha Sh milioni 250 ambazo zililipwa na TFF. Serikali ndiyo iliyokuwa ikimlipa mshahara kocha huyo.
Malinzi alisema Mkwasa atasaidiana na Kocha wa Zanzibar Heroes, Hemed Morocco, katika mechi nne zinazoikabili Stars ambazo ni kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) na Michuano ya Mataifa kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).
“Tayari tumemalizana na Yanga kuhusu kutupa Mkwasa, lakini hiyo haimaanishi kwamba ataachana na Yanga. Ataendelea na kazi yake Yanga na kwetu pia. Atalipwa kama alivyokuwa akilipwa Nooij na kupewa kila kitu,” alisisitiza Malinzi.
Kwa mantiki hiyo, Mkwasa atakuwa analipwa mshahara wa Sh milioni 25. Nooij aliiongoza Taifa Stars katika mechi 18 na kubahatika kushinda tatu tu na kufungwa tisa.
Kibarua cha kwanza cha Mkwasa kitakuwa Julai 4, mwaka huu wakati Taifa Stars itakaporudiana na Uganda ugenini kufuzu Chan hapo mwakani. Ikumbukwe Taifa Stars ilifungwa mabao 3-0 nyumbani, hivyo itahitaji mabao 4-0 ili kusonga mbele.

Note: Only a member of this blog may post a comment.