Friday, May 15, 2015

Anonymous

KIMENUKA! SIMON Msuva amvaa Hans Poppe wa SIMBA SC!

Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.
Wilbert Molandi na Shaban Mbegu
WAKATI Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe akiwa na matumaini makubwa ya kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva atatua Msimbazi kama ambavyo amekuwa akinukuliwa hivi karibuni, Msuva amekuja juu na kumjibu kiongozi huyo.


Wiki iliyopita, Hans Poppe alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa ana uhakika Msuva atatua Simba kwa kuwa mchezaji huyo ana mapenzi na klabu hiyo, huku mara kadhaa pia ikielezwa kuwa wazazi wa mchezaji huyo ni wanazi wakubwa wa Simba.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Msuva alisema kuwa soka ni ajira yake na ndiyo inayomuingizia kipato lakini kwa sasa hafikirii kuihama Yanga kisha kujiunga na Simba na badala yake anachowaza ni kusonga mbele zaidi.

Kuhusu madai ya Hans Poppe alisema hakuna kitu kama hicho, labda Hans Poppe anazungumza kwa ajili ya kujifurahisha kwa kuwa yeye bado ni mchezaji wa Yanga ambaye ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi.

“Hakuna kitu kinachonikera kama Hans Poppe kuongea kwenye vyombo vya habari kuwa mimi ni shabiki wa Simba, kitu ambacho siyo sahihi, ni vema akalijua hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe.
“Kikubwa anachotakiwa kukifahamu ni kuwa, mimi ni mchezaji wa Yanga, bado nina mwaka mmoja kwenye mkataba wangu, asitarajie kabisa mimi kwenda Simba hivi sasa.

“Mimi ninafikiria kucheza kimataifa zaidi na siyo tena hapa Bongo, ni ndoto nilizokuwa nazo na ninaomba Mungu anijaalie nizitimize, nikitoka Yanga basi niende kucheza soka nje ya nchi na siyo Simba,” alisema Msuva.Upande wa pili, siku chache baada ya Msuva kurejea kutoka Afrika Kusini ambako alikwenda kwa kutoroka kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka katika timu ya Bidvest Wits, kuna mazito yameibuka.

Katibu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, ameliambia Championi Ijumaa kuwa hatma ya mchezaji huyo juu ya kitendo chake cha kutoroka itajulikana leo Ijumaa baada ya uongozi kukaa kumjadili jana na leo.

“Kesho (leo) ndiyo tutakamalisha kila kitu na kutoa tamko juu ya nini tulichokiamua, tumeamua hili suala tuliangalie kwa umakini mkubwa kwa kuwa ndani yake kuna biashara, nidhamu na sheria,” alisema Dk Tiboroha na kuongeza:
 
“Pia jana (juzi) kabla ya kuondoka kwenda Afrika Kusini na Taifa Stars, tulimwita hapa na kupitia maelezo yake aliyotoa kwenye kamati ya kwanza na baada ya kusoma alithibitisha kila kilichoandikwa ndicho alichojitetea.”

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.