Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe amesema iwapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anataka kugombea urais kupitia chama hicho afuate taratibu za chama ikiwamo kutangaza mali zake.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la
Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia
mtu anayetaka kujiunga ACT – Wazalendo ikiwa atafuata taratibu
zilizowekwa na chama hicho.
“Naomba
niwaambie Watanzania kwamba ACT siyo chama cha kumtengenezea mtu
mazingira ili agombee urais, lakini kama Lowassa anataka kugombea urais
kupitia huku lazima atangaze mali zake na kueleza wapi amezipata kama
taratibu za chama zinavyosema,” Zitto.
Zimekuwapo taarifa kwenye vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wagombea akiwamo Lowassa
ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, wana mpango wa kutimkia ACT
iwapo watakatwa majina yao katika mchujo wa wagombea.
Kwa mujibu wa habari hizo, ACT –
Wazalendo imepewa fedha na Lowassa ambazo inatumia katika mikutano hiyo
kumwandalia nafasi ya kuwania urais, madai ambayo pande zote
zimeyakanusha.
Akizungumzia taarifa hizo kwenye mkutano
huo, Zitto alisema chama chake kinaongozwa kwa kufuata taratibu na
kitampokea yeyote atakayefuata taratibu hizo.
Kiongozi huyo ambaye hivi karibuni
alitangaza mali na madeni yake, alisema iwapo Lowassa atataka kujiunga
na chama hicho itambidi atangaze mali zake na kueleza jinsi
alivyozipata, kama yeye alivyofanya.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kauli ya Zitto, msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema: “Hakipo kitu kama hicho na hakitakuwapo, hatujui habari hii inatoka wapi? Mzee (Lowassa)
amekuwa akitumikia CCM maisha yake yote tangu enzi za TANU … yupo na
anaendelea kutumikia kifungo chake. Maisha yake yote ni mtumishi wa
chama.”
Lowassa pamoja na makada wengine watano
wa chama hicho walipewa adhabu ya onyo kali baada ya Kamati Kuu ya CCM
kuwatia hatiani kwa kuanza kampeni za urais mapema na kukiuka maadili ya
chama.


Note: Only a member of this blog may post a comment.