Monday, April 27, 2015

Anonymous

Yanga yaifuata Etoile kwa style hii..!

Na Nicodemus Jonas, Dar es Salaam
KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuondoka usiku wa Alhamisi kwenda Tunisia, kwa ajili ya kuwavaa Etoile du Sahel katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao utaamua hatima ya Yanga ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo. Mtanange huo utapigwa Jumapili, Mei 3, mwaka huu.


Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, kikosi hicho kinatarajia kutumia ndege ya Emirates, ambayo ni mali ya kampuni kutoka nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E).

Yanga inawafuata wababe hao ikihitaji ushindi wa lazima au sare ya kuanzia mabao mawili ili kutinga hatua ya mtoano, kufuatia sare ya bao 1-1 iliyoipata katika mchezo wa kwanza wiki moja iliyopita, vinginevyo ‘gundu’ la miaka 17 ya kutofuzu hatua ya makundi kwenye michuano mikubwa Afrika itakuwa imewaganda na kujipanga upya msimu ujao.

Kipa tegemeo kwa sasa, Ally Mustapha ‘Barthez’ ameeleza hofu yake na kusema wana kibarua kigumu kutokana na aina ya matokeo waliyoyapata na kuongeza kuwa ni lazima waongeze umakini, hasa katika safu ya ushambuliaji.

“Ni mchezo mgumu kwetu, hasa ukizingatia matokeo tuliyoyatapa, lakini kila kitu kinawezekana. Kama waliweza kutusumbua kiasi kile ugenini, unadhani itakuwaje kwao?” Alihoji kipa huyo wa zamani wa Simba na kuongeza:
“Of course’ tunahitaji umakini zaidi, hasa safu ya ushambuliaji, kila fowadi wao ni hatari na huwezi kusema utamchunga mmoja, wote wanatakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi.”


Mshindi katika mchezo huo, atafuzu hatua ya mwisho ya mtoano kabla ya kufuzu hatua ya makundi, ambayo mara ya mwisho Yanga kufika hatua hiyo ilikuwa mwaka 1998, kwenye michuano ya Klabu Bingwa (sasa Ligi ya Mabingwa).

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.