Wednesday, December 21, 2016

Unknown

TANESCO YATANGAZA KUTOA UMEME WA UHAKIKA BUNGENI

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuwa watalipatia Bunge la Tanzania laini ya umeme wa uhakika kutokana na mradi wa backbone.

Hayo yalibainishwa na Msimamizi wa kituo cha kupozea umeme cha Zuzu mjini Dodoma, Joseph Mongi alipokuwa akizungumza na wahariri waliotembelea miradi ya umeme. Mongi alisema Bunge litapatiwa laini yao ili kuliwezesha kuwa na umeme wa uhakika na wa kuaminika, tofauti na ilivyo sasa kabla ya kuja kwa backbone.

“Dodoma tunazo laini maalumu kwa maeneo ya mashine za maji, ofisi za serikali, chuo cha Udom, hospitali kuu ya mkoa na za wilaya za mkoa huu,” alisema.

Alisema wamekidhi mahitaji na wanao uwezo wa kuhimili mahitaji ya serikali yote ikihamia Dodoma. “Siyo mahitaji ya serikali mpya tu, bali hata wawekezaji wa viwanda watakaohitaji kufungua viwanda katika makao makuu ya Tanzania,” alisema.

Katika hatua nyingine, mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa backbone, unaingia katika rekodi leo wakati laini nzima ya umeme huo itakapowashwa. Meneja wa Ujenzi wa laini hiyo ya backbone, Oscar Kanyama, alisema laini ya Dodoma hadi Singida inawashwa leo. Kanyama alisema kwamba kuwashwa kwa kipande hicho, kutafanya mradi wote wa kilovolti 400 kufanya kazi.

“Kesho tunawasha laini ya Dodoma hadi Singida na hivyo sasa laini zote zitakuwa zinafanya kazi”, Kanyama aliwaeleza wahariri wanaotembelea mradi huo kuanzia Iringa hadi Shinyanga. Mradi huo wenye urefu wa kilometa 670, una vituo vinne vya kupozea umeme vya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga.

Laini za Iringa hadi Dodoma na Singida hadi Shinyanga, zilikuwa zimewashwa ikibaki ya Dodoma hadi Singida inayowashwa Leo.
Kanyama alisema kuwashwa kwa kipande hicho kutasaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.