Thursday, April 14, 2016

Anonymous

Tukio la AJABU Jijini Dar! Maiti Abadilishiwa Ndugu Muhimbili

IMG_2514
Ndugu wakiwa katika Hospitali ya Muhimbili.
DAR ES SALAAM: Ni tukio la ajabu! Simulizi vinywani mwa wakazi wa Jiji la Dar ni lile tukio la kusikitisha la mwili wa marehemu kukabidhiwa watu wasio ndugu na kwenda kuuzika kwao huku ndugu wakiambulia patupu licha ya kufika mochwari na jeneza, AMANI lina mzigo wote. 

Tukio hilo la aina yake lilijiri Aprili 11, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar ambapo familia ya Theodory Chivumile wa Ukonga- Gerezani kuukosa mwili wa Janeth Mtonga Theodory (52) kwa kuambiwa kuwa, ulichukuliwa na familia nyingine na kwenda kuuzika, Usangi mkoani Kilimanjaro

TWENDE HATUA KWA HATUA
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Raymond Theodory siku hiyo familia walipanga kufanya mazishi maana mpendwa wao alifariki dunia Ijumaa ya Aprili 8, mwaka huu kwenye hospitali hiyo.
“Lakini katika hali ya kushangaza huku waombolezaji wakiwa nyumbani wakisubiri mwili ili kuuaga, tulifika Muhimbuli tukaambiwa mwili wa mama umechukuliwa na ndugu zake.”
IMG_2504 
Jeneza likiwa tupu ndani ya gari.
MSHANGAO MKUBWA
“Tulishangaa sana! Ndugu zake akina nani wakati ndiyo sisi! Wakasema ndugu waliouchukua mwili wameusafirisha Kilimanjaro kwa mazishi, tukazidi kuchanganyikiwa,” alisema mtoto huyo.

MSIMAMO WA FAMILIA
Aliendelea: “Bado hili tukio halituingii akilini, sidhani kama wale ndugu walishindwa kuutambua mwili wa marehemu wao na kumchukua marehemu wetu. Ninafikiri ni uzembe tu uliofanyika maana marehemu wote huwa wanawekewa majina, wetu alikuwa anaitwa Janeth wao Amina, hapo mtu anaweza kuchanganya vipi? Tunaomba  suala hili lichunguzwe.”

NDUGU WENGINE
Gazeti hili pia lilifanikiwa  kuzungumza na mume wa marehemu aitwaye Theodory Chivumile ambaye hakupenda kupigwa picha kutokana na sababu binafsi, naye alionesha kushangazwa na tukio hilo lakini alisisitiza kwamba, wao kama familia hawahusiki kwa lolote na kilichotokea, kikubwa wanamtaka marehemu wao.
DSC_0693
Ndugu wakiwa msibani.
WIFI WA MAREHEMU
Luciana Saulenda ni wifi wa marehemu ambaye alionesha masikitiko yake makubwa na kusema haya:
“Sisi ni Wakristo, kwa hiyo marehemu wetu amekwenda kuzikwa kwa taratibu zingine na tutalazimika kumzika tena kwa taratibu zetu baada ya kufukuliwa. Kwa kweli si sahihi kilichofanyika. Tumeumia sana.”

MUHIMBILI WANASEMAJE?
Kwa upande wa uongozi wa Muhimbili walisema ndugu waliofanya makosa ni wale walioanza kwenda kuuchukua mwili wa marehemu ambao si wa kwao na kwenda kuuzika bila kuuhakiki kwanza.
“Ile familia nyingine ni Waislam na ndiyo walisababisha haya yote maana walimchukua marehemu bila kumkagua kuwa ni wa kwao na kwenda kumzika. Nadhani ni kwa sababu ya utaratibu wao.
“Lakini tumeshawasiliana nao, leo (Jumatatu) gari letu limekwenda mkoani Kilimanjaro, kesho (Jumanne) tutamrudisha marehemu na kumkabidhi kwa ndugu zake kwa ajili ya taratibu zingine za mazishi,” alisema Dk. Mosha mmoja wa viongozi wa kitengo cha mochwari hospitalini hapo.
IMG-20160412-WA0001 
Marehemu Janeth enzi za uhai wake.
Hadi tunakwenda mitamboni, ndugu wa marehemu Janeth walidai wanasubiri mpaka wakabidhiwe ndugu yao ndipo wafanye taratibu zingine za mazishi huku msibani nyumbani, meza ya kuweka jeneza wakati wa kuuaga mwili na mapambo mengine vikiendelea kuwepo.
Kuna taarifa kwamba, jeneza walilokwenda nalo kwa ajili ya mwili, lililala kwenye gari na muda mwingi ndugu hao walikuwa wakipiga simu kwa wahusika wa Muhimbili kuulizia wa Kilimanjaro wamefikia wapi katika kuurudisha mwili wa ndugu yao, Dar.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.