Tuesday, March 8, 2016

Anonymous

Stendi ya MSAMVU, Morogoro Yatakiwa Kumalizwa Haraka


Seleman Jafo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
SULEIMANI Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kusimamia vyema ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi iliyopo Msamvu, anaandika Christina Raphael.
Jafo pia amesema, halmashauri hiyo inapaswa kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika mapema Juni mwaka huu. Ametoa agizo hilo leo wakati akikagua ujenzi wa stendi hiyo unaoendelea katika hatua ya kwanza.

Amesema kuwa, ni vema ujenzi huo ukakamilika Juni katika hatua ya kwanza kwa mujibu wa mkataba ili wafanyabaishara warudi maeneo yao ya biashara kama awali.

Hata hivyo, aliwataka wafanyabishara na wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwa ujumla kuchangamkia fursa ya kibiashara iliyopo katika stendi hiyo mpya kwa kukodisha maeneo hayo.

Lakini pia ameagiza halmashauri zingine nchini kubadili mtazamo na kuiiga Manispaa ya Morogoro kwa kuanzisha ujenzi wa kitega uchumi kikubwa kitakachowasaidia katika masuala mbalimbali ya kuendesha halmashauri yao ikiwemo manunuzi ya mahitaji elimu.

Pia aliwaagiza viongozi wa manispaa kuhakikisha wanasimamia vyema makusanyo ya mapato ya stendi hiyo itakapokamilika na kuhakikisha hakuna mianya ya rushwa.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo Injinia Stanley Mhapa, Meneja wa Mradi wa Msamvu Properties co. Ltd amesema, mradi huo uliopo katika hatua ya kwanza umefikia asilimia 68 ya kukamilika tangu ujenzi huo ulipoanza Februali mwaka 2015.

Mhapa amesema mradi huo wenye awamu ya kwanza na ya pili unagharimu kiasi cha Sh. 40 Bil ambapo mpaka sasa tayari Sh. 3 Bil zimetumika ikiwa ni kati ya Sh. 9 Bil zilizotengwa kwa ajili ya awamu hiyo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.