Tuesday, March 8, 2016

Anonymous

MAKONDA Asusiwa ‘Daladala za Bure’


Abiria wakigombania daladala wakati wa jioni
WAKATI utekelezwaji wa agizo la Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kindondoni ukianza kutekelezwa jana, walimu wameususa, anaandika Faki Sosi.
Uchunguzi wa mtandao huu uliofanywa jana jioni kwenye daladala mbalimbali jijini Dar es Salaam umeonesha kwamba, uitikiaji wa agizo hilo haujazingatiwa kutokana na sababu mbalimbali.

Miongoni mwa sababu hizo ni hofu ya walimu kunyanyaswa, kudhalilishwa na hata kutolewa lugha chafu kutoka kwa makondakta wa daladala lakini pia si miongoni mwa madai yao kwa serikali.

“Katika daladala hili tangu asubuhi hakuna mwalimu aliyepanda na kuonesha kitambulisho kama ni mwalimu,” anasema Juma Mpimba ambaye ni kondakta wa daladala linalofanya safari zake kutoka Kawe kwenye Mawasiliano na kuongeza;

“Sitarajii kuona mwalimu akipanda kwenye dalalada hili halafu aoneshe kitambulisho eti asilipe nauli huku mtoto wake wa kumzaa alipe nauli.”

Simion Mkude ambaye ni kondakta wa daladala lifanyalo safari zake kutoka Mawasiliano kwenda Posta anasema kwamba, tangu aanze kufanya kazi asubuhi mpaka jioni, hakukutana na mwalimu aliyedai kutolipa nauli.

“Mimi sijakutana na mwalimu yoyote ambaye hajalipa nauli, kuna wengine tunawajua lakini wamelipa nauli zao. Unajua hili ni jambo lisilo rahisi,” amesema.

Alipoulizwa sababu za walimu hao kutoa nauli licha ya kuwepo kwa agizo la Makondo, Mkude amesema, wao wanajiheshimu na wanaogopa misukosuko yetu.
“Ikiwa wanafunzi ambao hulipa nusu hasara tunawaacha itakuaje walimu ambao hawalipi chochote, kwanza tunaweza tusiwajue lakini tukiwajua tutakuwa tunawaacha.

“Tutakuwa tunawaambia kwamba ndani wamejaa wenzenu hivyo tunapakia wenye pesa zao. Mimi naami kwamba, wazo hilo sio zuri na ni la uzalilishaji,” amesema.

Hata hivyo, baadhi ya makonda walidai kwamba, hakuna sababu ya walimu kutolipa pesa ya nauli kwa kuwa nao wana mishahara kama walivyo wafanyakazi wengine.

“Walimu wana mishahara kama wafanyakazi wengine, issue (hoja) si kuwa walimu hapa hoja ni kazi kwa kuwa hata ualimu ni kazi walioamua wenyewe kuisomea kama walivyosomea madaktari, wajenzi na wengine.

“Wakati mwingine walimu wana mishahara mikubwa kuliko wafagiaji huko mjini, wapo waokota makopo barabarani nao wanalipa nauli, kama ni hivyo kwanini mwalimu naye asilipe? Wawaongezee mishahara wasikwepe jukumu lao.” Anasema Zuberi Msonza ambaye ni kondakta wa daladala linalofanya safari zake kutoka Makumbusho kwenye Makongo Juu.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kinzudi, Makongo Juu aliyeomba kuhifadhiwa jina lake amesema kuwa, hatotoa kitambulisho ili apande bure.
“Hata siku moja siwezi kutoa kitambulisho ili nipande bure, kwanza nitaanzaje?” amehoji na kuingeza;

“Watu wote kwenye daladala watakuwa wanakuangalia wewe halafu ukute konda naye fyatu ndio kabisa,” amesema.
Agizo la Makonda kwamba walimu wapande bure daladala jijini Dar es Salaam linakumbana na dhoruba kali kutoka kwa wamiliki wa daladala, makondakta, wananchi na hata walimu wenyewe.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.