Watu zaidi ya 15 wamedaiwa kukivamia kituo cha redio cha Hits FM cha visiwani Zanzibar na kukiteketeza kwa moto.
Watu hao wanadaiwa walikuwa kwenye gari aina ya Noah waliyoipaki nje
ya ofisi hizi, kuwashambuliwa walinzi na kuwazidi nguvu kabla ya kuingia
kwenye studio za redio.
Tukio hilo limetoa usiku wa kuamkia Alhamis hii, saa saba na dakika 40.
Mtangazaji wa kituo hicho, Sophy Dalah ameiambia Bongo5 kuwa watu hao
walipoingia walimshikilia mtangazaji wa zamu na kumwekea matambala
mdomoni kumzuia asipige kelele.
“Watu hao walikuwa wamejifunika sura zao kama Ninja, walimwambia ‘uko
chini ya ulinzi kwa wakati huu tunaomba ushuke kwenye kiti cha
utangazaji na tunachokuambia tunaomba ufuate,” amesema mtangazaji huyo
wa kipindi cha Power Artist kinachoruka kwenye kituo hicho.
“Wakamfunga uso, wakamfunika ili asijue nini kinachoendelea
wakamwekea matambala mdomoni hatimaye wakamtoa nje. Walimpiga piga
mapanga lakini sio kwa kumuumiza, bali walikuwa wakimtishia tu,”
ameongeza.
Amesema watu hao wamechoma studio ya kurushia matangazo na ya kufanyia utayarishaji wa vipindi.
Hata hivyo amesema bado hawajajua sababu ya watu hao kukivamia kituo hicho na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi.
Ameongeza kuwa uongozi wa kampuni hiyo umewapa likizo ya kipindi kisichojulikana.
Note: Only a member of this blog may post a comment.