Mwanafunzi wa Kidato cha Pili, Jofrey Robert Mwakatenya anatuhumiwa kuuawa kikatili na baba yake mzazi, Robert Mwakatenya baada ya kumkuta akiwa na barua ya mapenzi, inayodaiwa aliandikiwa na rafiki wake wa kike.
Mzazi huyo ambaye ni mfanyabiashara na
mkazi wa eneo la Majengo ‘D’ Manispaa ya Sumbawanga, anadaiwa kumwadhibu
mwanafunzi huyo, ambaye ni mtoto wake wa kwanza kwa kumpiga ngumi na
mateke mfululizo kwa zaidi ya saa tatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda
alithibitisha tukio hilo, lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili
iliyopita. Alisema bado wanamtafuta mtuhumiwa huyo kwani baada ya
kufanya kitendo hicho alitokomea.
Mwenyekiti wa Serikali Majengo D, Antony Nyambo alidai kuwa mzazi huyo alikuwa na tabia ya kumwadhibu mwanawe huyo, akimtuhumu kuwa ni mtoro wa shule .
“Nilitaarifiwa
juu ya kisa hiki Jumapili saa mbili asubuhi baada ya kutoka katika
ibada na raia mwema, ndipo niliamua kufika nyumbani kwa marehemu,
nilimkuta akiwa amelazwa chumbani, nilipomfunua niliona akiwa ametapakaa
vumbi mwili mzima huku akiwa amevaa nguo ya ndani tu,”
Inadaiwa kuwa usiku huo wa tukio,
mtuhumiwa alianza kumwadhibu kumpiga ngumi na mateke kuanzia saa mbili
usiku hadi usiku wa manane.
Mtoto huyo baada ya kupata kipigo hicho,
alizimia ambapo baba yake alimwagia maji mwilini hadi akazinduka, kisha
akamwamuru alale chumbani humo pamoja na mdogo wake.
Mzazi wa mtoto huyo alidamka alfajiri na kwenda kwenye chumba walicholala watoto hao na kugundua kuwa Jofrey alikuwa mfu.
“Ndipo
baba huyo alipoaga nyumbani hapo, akidai kuwa anaenda kutafuta gari ili
Jofrey aweze kupelekwa hospitalini kwa matibabu. Mzazi huyo hakurudi
tena nyumbani kwake hadi sasa,” .
-HABARILEO


Note: Only a member of this blog may post a comment.