Uamuzi
wa Rais John Magufuli kuunganisha wizara kutoka 30 hadi kuwa 18 na
idadi ndogo ya mawaziri, hautasababisha kupunguzwa kwa watumishi, hasa
makatibu wakuu, Ikulu imeeleza.
Juzi,
Rais Magufuli alitangaza kuunganisha wizara na kuunda Baraza la
Mawaziri lenye wizara 18 kutoka 30 za Serikali ya Awamu ya Nne, uamuzi
ambao umeibua hofu kwa baadhi ya watumishi kuwa panga hilo linaweza
kuwakumba makatibu wa wizara zilizopunguzwa.
Jana,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alieleza kuwa Serikali
itafanya mgawanyo mpya wa majukumu kwa watumishi wote na suala la
kuwapunguza kazi halifikiriwi kwa sasa.
Balozi
Sefue alisema fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2015/16,
zitapelekwa kwenye kila wizara husika, hata kama itakuwa imeungwanishwa
na nyingine na kuunda wizara moja.
Katika
mabadiliko na uundaji wa baraza hilo, Dk Magufuli ameunganisha baadhi
ya wizara, huku akizihamisha baadhi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na
kuzipeleka Ofisi ya Rais na nyingine kuziondoa kwenye kujitegemea na
kuziingiza Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa
hatua hiyo, watumishi wa wizara kati ya mbili hadi tatu watajikuta
wakiwa katika wizara moja pamoja na waliokuwa makatibu wakuu wa wizara
hizo, jambo litakaloongeza idadi ya watumishi na baadhi yao huenda
wakajikuta wakifanya kazi zinazofanana au kukosa kitu cha kufanya.
“Baada
ya baraza kuundwa lazima kutakuwa na realignment ya watumishi
(kuunganisha upya shughuli zinazoshabihiana). Kuna mambo mengi, hata
ofisi inabidi tuzipange upya. Hiyo ipo wazi kwa watumishi, sidhani kama
kuna ulazima wa kupunguza idadi yao zaidi ya kuwapangia majukumu
mengine,” alisema Sefue.
Alisema mtumishi wa umma hajaumbwa kuwa mtumishi wa wizara moja tu maisha yake yote.
“Kwa
hiyo, tutatazama kama wanaweza kuwa redeployed (kupangwa upya) vipi.
Wale ambao hawatahitajika kwa ukubwa wa baraza la mawaziri lililopo,
tutaona wanaweza kutumika vizuri zaidi sehemu gani,” alisema.
Alipoulizwa
kama kuna utaratibu wowote wa kupunguza wafanyakazi alisema:
“Hatupunguzi, labda tuone mtu hahitajiki kabisa. Lakini, kwa wakati huu
hatuna msingi wa kusema kuna watu hatutawahitaji. Baada ya mawaziri
kuapishwa na kuanza kazi tutaanza suala hili.”
Kuhusu
makatibu wakuu wa wizara ambazo zimeunganishwa na kuwa wizara moja,
Balozi Sefue alisema: “Nao ni hivyo hivyo. Bado kuna mambo mengi ambayo
wanaweza kupewa na wakafanya vizuri tu, wakati wa uamuzi huo bado
haujafika ila kwa sasa hatufikirii kuwapunguza.”
Kuhusu
mpangilio wa majukumu yao, Balozi Sefue alisema: “Ngoja uundwaji wa
baraza ukamilike tuone wapi watahitajika na hao ambao watabaki tuwafanye
nini. Uamuzi huo utafanyika baadaye.”
Akizungumzia
mgawanyo wa fedha za bajeti za wizara ambazo kwa sasa zimeunganishwa na
kuwa wizara moja, katibu huyo mkuu kiongozi alisema bajeti ya Serikali
ni kwa vitu maalumu, kwa hiyo kama kulikuwa na bajeti ya Wizara ya
Afrika Mashariki ambayo katika bajeti walikuwa na kazi inayohusu eneo
hilo, fedha ya bajeti hiyo itakwenda inakohitajika kwa ajili ya kufanya
kazi iliyokusudiwa licha ya wizara hiyo kuunganishwa.
“Yaani,
fedha hiyo itakwenda katika wizara mpya (iliyounganishwa na nyingine),
bajeti nayo itakwenda huko sanjari na wafanyakazi ambao nao watakuwa
katika wizara hiyo hiyo. Kwa maana hiyo, bajeti hiyo itatumika kama
kawaida,” alisema.
Rais
Magufuli alisema wakati akitangaza baraza lake la mawaziri kuwa ameamua
kuwa na wizara chache ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha za
Serikali.
Kutokana
na uamuzi huo, wizara zilizounganishwa ni ya Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Utumishi na Utawala
Bora, imeunganisha shughuli za Tamisemi zilizokuwa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Awali, Ofisi ya Rais ilikuwa na waziri watatu; Utawala Bora, Mahusiano
na Uratibu na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Nyingine ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ambazo zilikuwa mbili tofauti, chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Katika
Ofisi ya Waziri Mkuu, ipo Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Walemavu. Awali, Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira ilikuwa inajitegemea,
wakati ya walemavu ni mpya.
Mabadiliko
hayo yamepunguza idadi ya wizara zilizokuwa chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu ambazo ni Sera, Uratibu na Bunge, Uwekezaji na Uwezeshaji na
Tamisemi, zikiwa na mawaziri watatu na manaibu wawili.
Nyingine ni Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo awali kila moja ilijitegemea.
Wizara
ya Fedha sasa imeongezewa Mipango na sasa itaitwa Wizara ya Fedha na
Mipango. Pia, Wizara ya Viwanda na Biashara imeongezewa Uwekezaji. Suala
la masoko limeondolewa wakati Uwekezaji ilikuwa pamoja na uwezeshaji.
Kutakuwapo
pia na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda
na Kimataifa ambayo imeunganisha wizara mbili; Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa na ile ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Nyingine
ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, ambayo imechukua
majukumu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni matokeo ya
kuunganisha Afya na Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto.


Note: Only a member of this blog may post a comment.