Utekelezaji
 wa ahadi za Rais John Magufuli unazidi kushika kasi baada ya kuanza kwa
 mchakato wa kuanzisha mahakama maalumu ya kuwashughulikia mafisadi.
Jaji
 Kiongozi, Shaban Lila alisema jana kuwa tayari wadau mbalimbali wa haki
 jinai wameanza kukutana kuangalia namna ya kuanzisha mahakama hiyo kama
 sehemu ya utekejezaji wa ahadi ya Rais.
Akizungumza
 katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya kushughulikia mashauri nyeti ya 
jinai kwa majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alisema juzi walikuwa 
na mazungumzo na Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia mfumo wa 
uendeshaji wa mahakama hiyo.
“Tunaangalia
 tuianzishe kama mahakama huru au ifanywe ndani ya muundo wetu wa 
mahakama kwa kuipa kipaumbele maalumu. Lakini tunafikiria zaidi kama 
ingekuwa ni kitengo maalumu ndani ya Mahakama Kuu kitakachokuwa 
kikishughulikia mafisadi,” alisema Jaji Lila.
Hata
 hivyo, Jaji Lila hakutaja muda maalumu utakaotumika kumaliza mchakato 
wa kuanzisha mahakama hiyo, huku akisema unahusisha wadau wengi na 
unyeti wake unahitaji maandalizi makubwa.
Jaji
 huyo bila kutaja takwimu, alieleza kuwa kesi za makosa makubwa ya jinai
 zinaongezeka nchini ukilinganisha na miaka ya nyuma hasa zile 
zinazohusu utakatishaji fedha, ugaidi, usafirishaji wa dawa za kulevya, 
usafirishaji wa nyara za Serikali hasa wanyama hai na mazao yake na 
ufisadi.

 

 
 
 
 
Note: Only a member of this blog may post a comment.