Makongoro Oging’ na Mayasa Mariwata
SIMANZI! Watoto watatu wa familia tofauti wakazi wa Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam, wamekufa maji katika eneo la Bahari ya Hindi lijulikanalo kama Kondo Beach baada ya kuzidiwa na maji wakati wakiichezea meli mbovu iliyo ndani ya bahari mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa mmoja wa wazazi wa watoto
hao, vijana hao walimfuata mjukuu wake nyumbani wakimtaka kwenda kucheza
kama ilivyo kawaida yao, lakini baadaye alipata taarifa ya kufa maji
kwa vijana watatu.
Devota Komba, bibi wa marehemu Abel
Osmundi (11) aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi
Mtakuja, alisema watoto hao walimfuata mjukuu wake majira ya saa nne
asubuhi na mara nyingi siku za wikiendi, huenda kwa Wakorea ambao huwapa
vyakula na vinywaji kisha wanarudi nyumbani.
“Machale
yakanicheza nikawakataza wasitoke, baada ya muda nikajisahau wakaondoka
japo sikupata hofu sababu nilijua wameenda kwa Wakorea ambapo si mbali
na eneo tunaloishi.
Cha kushangaza wakiendaga huko huwa
kwenye saa sita wanarudi, lakini siku hiyo nikaona kimya hadi saa kumi,
akaja kijana mmoja na kutuambia tukatambue miili ya watoto wetu Kondo
Beach na kukuta mjukuu wangu kafariki, naiomba serikali iitoe hiyo meli
mbovu majini,” alisema.
Akieleza jinsi vifo hivyo vilivyotokea,
bibi huyo alisema walioshuhudia tukio hilo walimwambia kuwa watoto hao
watatu ambao wenzao wawili walioondoka nao nyumbani hawakujiunga kwenye
safari ya ufukweni, awali waliingia majini kuchezea meli mbovu ambayo
ipo katikati ya bahari, baada ya maji kuanza kujaa wakafanya juhudi za
kujiokoa lakini hazikuzaa matunda.
Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto
Raphael Agustino (7) aliyejitambulisha kwa jina la Sikitu Joseph alisema
anashindwa kuamini kilichotokea, kwa vile hakuwahi kumsikia mwanaye
hata siku moja akizungumzia mambo ya beach.
Baba mzazi wa mtoto Andrew Masumbuko (11) aliyejitambulisha kwa jina la
Masumbuko Donatus alisema naye alisikitishwa na kifo cha mtoto wake
kipenzi, akisema mwanaye hakuwa na tabia za kutembelea ufukweni.
Watoto hao walizikwa Jumapili iliyopita
katika Makaburi ya Kondo huko Kunduchi Beach, vifo vyao vimeacha simanzi
kubwa kwa wakazi wa eneo hilo huku wakitoa wito kwa serikali kuiondoa
meli hiyo mbovu ufukweni hapo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.