CHANDE ABDALLAH
SHERIA yachukuwa mkondo wake. Hilo
limejidhihirisha baada ya Henry Domzalski (66), raia wa Marekani
aliyedaiwa kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya bangi mwaka 2013
nyumbani kwake Msasani Beach jijini Dar kujikuta akihenyeshwa mahakamani
na hatimaye kuhukumiwa miezi mitatu jela.
Akitoa hukumu hiyo, hakimu Kasailo
alisema kuwa baada ya mahakama kupitia ushahidi na upande wa utetezi na
kujiridhisha, imemtia hatiani Henry kwa kosa la kukamatwa na madawa ya
kulevya aina ya bangi kiasi cha kilo 135.67 nyumbani kwake hivyo
mahakama hiyo inamhukumu kutumikia miezi mitatu katika Gereza la Keko
bila faini.
Hata hivyo wakili wa upande wa utetezi,
Hudson Ndusyepo aliiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa kile
alichodai kuwa hilo ni kosa la kwanza kwake pia ni raia wa kigeni ambapo
hakimu huyo alisema kuwa rufaa ipo wazi kwa mtuhumiwa huyo kama
hajaridhika na hukumu hiyo.
Akiwa mahakamani hapo, mwandishi wetu
alishudia Henry akiwa amezungukwa na askari magereza na kasha
kusindikizwa kwenda kukwea karandinga tayari kuanza kutumikia kifungo
chake katika gereza la Keko.
Henry aliwahi kuwa mfanyakazi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Henry Domzalski (64) na kustaafu mwaka 2008.
Note: Only a member of this blog may post a comment.