Aliyekuwa Mgombea Ubunge jimbo la Mbagala kwa tiketi ya CUF, Kondo Bungo
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ofisa Haki za Binaadamu na Sheria wa CUF, Mohamedi Mluya amesema kuwa, jopo la wanasheria wa chama hicho wamejiandaa kufungua kesi ya kupinga matokeo ya majimbo hayo wakidai walishinda.Akitaja majimbo hayo Mluya amesema kuwa ni Tabora Mjini, Newala, Pangani, Mtwara vijijini na Mbagala ambapo kulikuwa na uvunjaji wa sheria ya uchaguzi.
Amesema kuwa kasoro hizo ni matumizi ya fomu ambazo hazikujazwa kikamilifu, nyaraka zinazoonesha idadi ya vituo vya kupiga kura na idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura hazifanani pia hujuma za viongozi wa CCM, kuvamia vituo vya majumisho kinyume na utaratibu nyakati za usiku wa manane.
“Sisi wanasheria wa chama tunapinga matokeo hayo kutokana na kuwa uchaguzi wa kihuni ambapo maofisa wa tume ya uchaguzi katika majimbo hayo wametumika na CCM, pia tunaamini katika majimbo hayo sita tumeshinda,” amesema Mluya.
“Tumeshuhudi kuwa fomu namba 21b haikujazwa kikamilifu, kwa mfano wa Kata ya Ndevelwa ambapo zilizotumika kama fomu halali za matokeo ilhali hazina Jina la kituo cha kupiga kura, hazina majina ya mawakala, hapakuwa kuna sahihi za wamakala hao pia fomu hizo zilikuwa hazina ‘serial number’ ambapo matokeo yake yalikuwa yamembeba mgombea wa CCM,” amesema Peter.
Peter amesema kuwa, suala la Katibu Mkuu wa CCM Wilaya ya Tabora kuingia katika kituo cha majumuisho usiku wa manane kinyume na utaratibu kinaashiria wizi wa kura.
Mwenyekiti wa Vijana CUF Taifa Hamidu Bobali ambaye ni Mbunge Mteule wa Jimbo la Mchinga ameitaka mahakama kutenda haki kwa kuwaachia huru vijana waliokamatwa wakiwa wanasubiri matokeo ya wagombea wao katika vituo ya majimbo mbalimbali.
Hivi karibuni gazeti hili liliripoti malalamiko ya mgombea wa Jimbo la Mbagala, Kondo Bungo kuvurugwa kutokana na matokeo ya jimbo hilo kubandikwa kinyemela na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ambaye alikuwa ni msisimamizi mkuu wa jimbo.
Note: Only a member of this blog may post a comment.