Wapendwa leo ningependa tujadili juu ya usiri wa mali katika ndoa,Katika jamii ambayo imenizunguka kwa mwaka huu tu nimepata kuona jambo hili likijitokeza mara tano katika misiba tofauti tofauti iliyotokea na mingine ikiwa ni ya ndugu zangu jamaa na marafiki, na katika misiba hiyo bahati mbaya yote inawahusu wanaume ambao wametangulia mbele ya haki huku wakiwa wameacha watoto pamoja na wake zao.
Mbaya zaidi katika familia hizo hakuna yoyote hata wake zao anayejua Mali za hao waume zao ziko wapi zaidi ya Nyumba wanazoishi walizoachiwa na marehemu,moja ya msiba ulionishangaza na kunisikitisha sana ni kuona rafiki ya marehemu anajua Mali nyingi karibu kila kitu cha marehemu alichoacha kuliko hata mkewe na la zaidi marehemu ana watoto wakubwa tu ambao angeweza kuwaambia au kuwashirikisha mambo yake.
Ni wito wangu wanandoa tuache usiri usio na tija,mshirikishe mkeo au mumeo kwa Mali ulizonazo,tuambiane kweli,mpaka mtu unaamua kuingia katika ndoa ina maana umeridhika na huyo uliyemchagua,usiri hauna maana yoyote zaidi ya kuwatesa tu watoto na kuwaacha katika mateso makubwa,hakuna mwenye dhamana ya maisha akajua anaondoka lini duniani,hatukuja na kitu duniani na hatutaondoka na kitu vyote tutaviacha.
Wanaume wafundisheni wake zenu kutafuta ili wajue kuheshimu na kuvitunza vile vinavyopatikana kwaajili ya familia,msiwafungie wake zenu majumbani mwenu kama mifugo matokeo yake Mungu anapowachukua mnawaacha wanateseka na watoto wenu maana walizoea kuletewa kila kitu,na wakati mwingine hata zile Mali mlizoziacha zinapotea maana zinakuwa hazina msimamizi tena kwasababu kila kitu kiliendeshwa na mwanaume.
Nawatakia ndoa zenye furaha,amani na baraka tele, Mwenyezi Mungu awe nanyi daima.karibuni wote kwa mjadala zaidi.
By everlenk/JF
Note: Only a member of this blog may post a comment.