Akizungumza na waandishi wetu kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, Flora alisema amechoshwa na manenomaneno yanayosemwa juu yake na Emmanuel na kwamba kama mumewe huyo ameamua kumwaga ugali, yeye yupo tayari kumwaga mboga.
Mwimbaji huyo alisema kwamba kauli
aliyoitoa hivi karibuni kuwa anampenda mumewe na kwamba yupo tayari
kuishi naye haikutoka moyoni, isipokuwa alifanya hivyo kwa huruma tu,
kwa sababu mwanaume huyo ni mtu katili, mwenye roho mbaya na
asiyemuogopa Mungu.
“Mtu mwenyewe alimtelekeza mtoto (Liz)
kwa zaidi ya mwaka mmoja, ni mtu mbaya sana, sina mapenzi na Mbasha hata
kidogo, ni afadhali niolewe na chizi anayeokota makopo kuliko kurudiana
na mtu katili na mnyama kama huyo, namheshimu kama mzazi mwenzangu kwa
Liz,” alisema.
“Huyo mwanaume hafai kabisa, ni katili,
namfananisha na shetani, anajifanya mwema kwa watu wakati hajawahi
kuiomba msamaha familia, sikubaliani kabisa na hukumu ya mahakama,
ukweli anaujua kwamba alibaka na hata mkimtaka huyo binti mumhoji
nitamleta, isitoshe sasa hivi hata mtoto wake hamjali, hajui anasoma
vipi, hajawahi kulipa hata shilingi ya ada, mimi mwenyewe ndo nahangaika
kumlea mwanangu Liz ambaye anasoma kidato cha kwanza.
“Hastahili kabisa kuitwa baba sababu
mzazi mwenye akili hawezi kutelekeza familia hata kama tumegombana,
nimemwachia nyumba niliyojenga kwa pesa yangu na pesa zote aliweka
kwenye akaunti yake na zote nilimwachia lakini kashindwa kuihudumia
familia.”
Flora anajulikana kuwa na watoto wawili,
mdogo akiwa ni yule aliyezaliwa wakati wanandoa hao wakiwa katika mzozo
uliosababisha watengane hadi hivi sasa. Alipoulizwa kwa nini anadai
aliyekuwa mumewe kumtelekeza mtoto mmoja tu, badala ya wawili,
alifunguka.
“Huyu mwanangu mdogo hausiki naye
kabisa, tena asiwe anamtaja kabisa kwa sababu hamhusu, hajui hata
matumizi yake yakoje, mengine kaka achana nayo tu,” alisema Flora.
Mwimbaji huyo mwenye kipaji alipoulizwa
sababu za kufuta kesi ya kudai talaka, aliyoifungua hivi karibuni katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati anadai hamtaki na hawezi
kurudiana naye, alisema alifanya hivyo baada ya kushinikizwa na mtu
ambaye hata hivyo, alikataa kumtaja.
Flora alisema familia yake
haijaridhishwa kabisa na suala la kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili
mumewe kumalizika kwa kuachiwa huru na kwamba wanajipanga kwa ajili ya
kukata rufaa.“Hiyo kesi imeisha kisiasa, Mbasha aliwahi kukiri kuwa ni
kweli alifanya kitendo hicho, iweje leo aonekane hana hatia? Tutakwenda
kukata rufaa ili haki itendeke.”
Baada ya kuzungumza na Flora, mwandishi
wetu alimtafuta Mbasha kwa lengo la kumuuliza kuhusu madai ya mtoto yule
mdogo kutohusika naye kama alivyosema mkewe, naye bila ‘kutafuna
maneno’, alisema hata yeye hamtambui huyo mtoto mdogo, ila anaomba
arudishiwe mtoto wake mkubwa, Liz na maisha mengine yaendelee.
“Hata mimi simtambui huyo mwingine,
ninachoomba anirudishie tu mtoto wangu mkubwa Liz, huyo mwingine
sihusiki naye kabisa kama alivyosema, yeye (Flora) ndiye anajua mhusika
wa huyo mtoto, lakini si mimi na wala hajakosea kusema hivyo,
nililitambua hilo tangu zamani, anipe tu mwanangu wa kwanza,” alisema
Mbasha.
Imeandikwa na Brighton Masalu, Mayasa Mariwata na Gladness Mallya
Note: Only a member of this blog may post a comment.