Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando,amelazwa
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, huku
hali yake ikielezwa kuwa tete baada ya kuugua ghafla juzi nyumbani
kwake.
Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, amelazwa katika
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitalini hapo kwa ajili ya kupata
matibabu.
Mmoja wa wauguzi wa zamu katika kitengo hicho ambaye hakutaka kutaja
jina lake kwa madai siyo msemaji wa mgonjwa huyo wala hospitali, alisema
Marando alifikishwa hospitalini hapo juzi akiwa na hali mbaya.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa watu wa karibu na Marando hali yake
inaleta matumaini ikilinganishwa na alivyofikishwa hospitalini hapo
juzi.
“Alifikishwa
hapa jana usiku (juzi), mimi sikuwapo ila hali yake ilikuwa mbaya
lakini kwa mujibu wa ndugu zake amboa ndiyo wako naye hapa wanasema
anaendelea vizuri ikilinganishwa na juzi,” alisema.
Alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya hawawezi kuruhusu waandishi wa
habari kuchukua taarifa yoyote na kwamba hata mke wake amekataa kutoa
taarifa za mume wake hadi hapo atakapopona.
“Hata
mkienda hamuwezi kuongea naye chochote na tangu asubuhi ukimuuliza kitu
anakuangalia tu na anapotaka kuzungumza anabaki anaguna, kwa hiyo kwa
hali yake hawezi kuzungumza,” alisema muuguzi huyo.
Alisema wanamatumaini hali ya Marando itakuwa nzuri zaidi baada ya siku
mbili kwani kuna dawa wamempatia ambazo zinahitaji apumzike.
“Unajua
hawa wanasiasa wanakosa muda wa kupumzika kutokana na kazi zao na hata
hapa tunamuona anahamu ya kuzungumza chochote lakini hawezi kutokana na
hali yake ndiyo maana tunataka apumzike zaidi,” alisema.
Naye mmoja wa ndugu wa Marando ambaye pia hakutaka kujitambulisha jina
lake, alisema mwanasheria huyo aliugua gafla akiwa nyumbani kwake juzi
usiku.
“Jana
mchana hadi jioni (juzi) nilikuwa naye lakini nilishangaa kupigiwa simu
usiku kuelezwa kuwa aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na hata hivyo
hatujaweza kuzungumza naye zaidi ya kupewa taarifa za hali yake na mke
wake,” alisema ndugu huyo.
Alisema tangu wamempeleka hospitalini hapo bado hali yake ni mbaya ingawa anaendelea na matibabu.
Sababu za ndugu hao kuishia nje zilielezwa kuwa ni kutokana na hali ya Marando kutohitaji usumbufu wa watu kuingia wodini.
Miongoni mwa ndugu waliokuwa hospitalini hapo ni mama mzazi wa Marando
ambaye alikuwa amekaa nje akisubiri taarifa ya hali ya mwanaye.
Mtu mwingine wa karibu na Marando ambaye hakutaka kutaja jina lake
alisema, aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa hospitali ya
kwanza ambayo hata hivyo hakutaja jina na baada ya kumpatia huduma ya
kwanza walisema hawawezi kumtibu na hivyo kuhamishiwa Hospitali ya
Muhimbili.
“Hapa
hospitali walimleta usiku akaanza kupatiwa matibabu na hali yake
ilikuwa mbaya lakini baada ya kupatiwa matibabu inaendelea vizuri
kidogo,” alisema.
Kwa upande wa mke wake ambaye pia hakutaka kujitambulish jina alisema kuwa, hawezi kuzungumzia hali ya mumewe bila ridhaa yake.
Mkewe huyo alitoka wodini majira ya saa 11:00 jioni na kuwapatia ndugu,
jamaa na marafiki waliokuwa wamesimama nje ya jengo hilo taarifa ya
hali ya mumewe.
Alisema ni kweli mumewe ni mgonjwa lakini taarifa ugonjwa wake ataitoa mwenyewe.
“Ni
kweli mume wangu ni mgonjwa lakini siwezi kumzungumzia bila kibali
chake na kuna waandishi wengine wamekuja sijawapa taarifa. Huyu ni
mwanasiasa na mnafahamiana, akipona tu atazungumza mwenyewe kila kitu,” alisema na kuondoka eneo hilo.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Steven, alithibitisha kupokelewa Marando hospitalini hapo juzi saa 4:00 usiku.
“Ni
kweli Marando kalazwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anapata
matibabu lakini taarifa kamili ya ugonjwa wake unaweza kuipata kwa
mwenyewe wodini au kwa ndugu,” alisema Steven.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hana taarifa ya kuugua kwa Marando.NIPASHE

Note: Only a member of this blog may post a comment.