Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambaye amekuwa mstari wa mbele
katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu akimnadi mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema anaeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa, ameeleza
nafasi atakayokuwa nayo baada ya uchaguzi.
Akiongea katika mahojiano maaalum na Tido Mhando wa Azam TV, Sumaye
alieleza kuwa hajaahidiwa cheo chochote na upande wa upinzani na kwamba
uamuzi wake wa kuwasaidia ni kutaka kuongeza nguvu zaidi ya uzoefu
katika kuleta mabadiliko nchini.
Alisema kuwa ameamua kuwa mwanaharakati kama Ernesto ‘Che Guevara ‘de
la Serna, aliyefanya kazi ya kuleta mapinduzi katika nchi mbalimbali
ikiwemo nchi ya Cuba.
“Kwa sasa ninafanya kazi kama Che Guevara, nadhani hii ni nafasi
muhimu zaidi hasa kama hao watu watautumia ushauri wako,” alisema.
Sumaye alieleza kuridhishwa na kazi wanayoifanya Ukawa kwa kuwa
wameibua upinzani mkali dhidi ya CCM. Ingawa alisisitiza kuwa na uhakika
kuwa Ukawa watashinda katika uchaguzi huu kwa jinsi alivyoshuhudiwa
wananchi wengi wanaouunga mkono umoja huo, Sumaye alieleza kuwa endapo
hawatashinda bado watakuwa wamefanya kazi kubwa kwa kuwa serikali ya CCM
itakayoingia madarakani haitalala tena. Alisema upinzani waliokutana
nao mwaka huu utaiamsha CCM.
Sumaye alitangaza kujiunga na kambi ya Ukawa akitokea CCM na kueleza
kuwa amechukua uamuzi huo kwa nia ya kuongeza nguvu ya kuleta
mabadiliko.

Note: Only a member of this blog may post a comment.