Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
MUHIMBILI hali ni tete! Hayo ni maneno ya
baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Dar baada ya kubaini kwamba kuna mashine za vipimo kadhaa hospitalini
hapo zimeharibika.
Afisa mmoja hospitalini hapo ambaye alizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini kwa kuwa siyo msemaji, alisema vipimo vilivyoharibika kwa muda mrefu ni CT Scan na Mari Spaind ambavyo ni muhimu katika kupima magonjwa.
“Huu ni mwezi wa pili vipimo hivyo vikiwa vimeharibika, wagonjwa wanataabika sana na wengine wamekuwa wakienda hospitali binafsi kupimwa, lakini walio wengi wanashindwa kumudu gharama kwa kuwa ni kubwa,” alisema mtoa habari wetu.
Alisema kuna wagonjwa wanaotoka mikoani baada ya kupewa rufaa na wanapofika Muhimbili na kukuta hali kama hiyo, hukata tamaa.
Kaimu Ofisa Habari wa Muhimbili, Stephen John alipoulizwa alikiri kwamba mashine hizo ni mbovu.
“Hatua za makusudi zimechukuliwa kwa ajili ya kuzitengeneza na kazi hiyo imepewa Kampuni ya Philips. Kasi ya kuzitengeneza ni kubwa na muda mfupi ujao zitafanya kazi,” alisema.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Afya Dk. Seleman Seif Rashid (pichani) ili afafanue tatizo hili lakini hakupatikana.
Note: Only a member of this blog may post a comment.