Vijana wako bize kutafuta hela kwa kila mbinu, wenye haraka wakitumia silaha, ushirikina na hata utapeli, ili mradi kila mmoja anajitahidi kuhakikisha maisha yake ya leo yanakwenda sawa, huku akijiweka vizuri kuishika kesho yake isiingie mushkeli.
Husna Sajenti ambaye ni muigizaji wa filamu Bongo, ambaye ni mzazi mwenzie na mwanamuziki nyota wa muziki wa dansi, Charles Gabriel ‘Chalz Baba’ ni miongoni mwa vijana hao wa Kibongo ambao wako bize kuhakikisha fedha zinaingia ili maisha yaendelee, no matter what!
Habari njema kwa mashabiki wa Husna ni kwamba wiki chache zilizopita, binti huyo alijifungua mtoto wake wa pili (huyu hakuzaa na Chaz Baba) na hivyo kuzidi kuongeza idadi ya wanafamilia yake. Kwa jamii nyingi za Kiafrika, licha ya kiuchumi kujiongezea mzigo, lakini ujio wa kiumbe kipya katika familia ni jambo la kupongezwa!
Ingawa hata hivyo, maisha ya mtu ni yake binafsi, wakati mwingine siyo jambo baya kumshauri unapoona anachokifanya, ama hakiendi sawa kijamii, kiafya au hata kiutamaduni.
Akiwa na wiki moja tu tangu ajifungue, Husna ameonekana mara kadhaa akiwa katika matukio ya kisiasa yanayofanyika usiku, lakini akiwa peke yake. Maana yake ni kuwa mwanaye mchanga, humuacha peke yake nyumbani, au huenda naye na kumkabidhi mtu mwingine anayekuwa mbali na alipokaa.
Ni kweli kuwa katika maisha ya uzungu ambayo vijana wengi wa Kiafrika wanajaribu kuishi, hili ni jambo la kisasa, tofauti na mama zetu ambao mila ziliwalazimisha kuamini kuwa mtoto hawezi kuachwa peke yake hadi amalize siku 40 tangu azaliwe!
Na upo ushahidi wa mazingira kuwa wasanii wanaojitokeza katika mikusanyiko ya vyama vya siasa vilivyo katika kampeni hivi sasa, wanalipwa. Yes, ni wakati huu wa kuchangamka, kwa sababu usipotumia nafasi yako, utachekwa!
Hata hivyo, pamoja na uchu wetu wa fedha, sidhani kama ni jambo jema kwa afya ya mtoto, tena wa Kiafrika, mama mzazi kwenda kwenye matukio ya usiku na kukaa huko hadi majogoo!
Na huenda hayo ni matukio ambayo tunamuona, kwa sababu hata sisi pia huwepo huko. Kama ishu ni kwa sababu ya mkwanja, kwamba analipwa sifikiri kama hakuna maeneo mengine yenye fedha yanayoweza kumvutia na kwenda nyakati za usiku!
Kama hivi ndivyo, nadhani dada huyu anahitaji ushauri kidogo, kwa namna ya kumkumbusha kuwa kila kitu na wakati wake, ndiyo maana kuna muda wa kibaolojia ambao mwanamke anabeba mimba.
Vivyo hivyo, anao muda anaopaswa kumlea kwa karibu mwanaye, kwani tunajua ataacha kunyonya, ataanza kutembea kabla ya kuanza kujitegemea.
Kumuacha mtoto katika kipindi ambacho anahitaji joto la mama kwa ukaribu ni kumnyima haki yake. Kama ishu ni hela, mbona zipo tu maana alizikuta na ataziacha. Kama zimekuja kipindi ambacho yeye yupo katika malezi, ni kumshukuru Mungu tu kwani kila mtu na riziki yake inayokuja kwa wakati wake.

Note: Only a member of this blog may post a comment.