Na Makongoro Oging’
KAA chonjo! Mfanyakazi wa ndani ‘hausigeli’, Sheila
Chacha (pichani) aliyekuwa akifanya kazi kwa Abraham Jullu maeneo ya
Tegeta-Wazo, Dar anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Mkoa wa Mwanza
akidaiwa kuiba mtoto wa tajiri yake aitwaye Coletha (1/8) jijini Dar.
Mfanyakazi wa ndani ‘hausigeli’, Sheila Chacha anayetuhumiwa kwa kuiba mtoto.
Akizungumza na gazeti hili juzi, baba mzazi wa mtoto huyo, alisema
mfanyakazi huyo wa ndani alitoweka na mtoto huyo Septemba 22, mwaka huu
na haikujulikana alipoelekea.Aliendelea kusema kwamba, walipoulizia watoto wengine alipo mfanyakazi huyo, walisema aliondoka na mtoto na hakurudi.
Walimsubiri lakini hakurudi hadi kesho yake ndipo wakaenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Wazo Hill Dar na kuandikiwa jalada lenye namba ya kesi WH/8094/2015.
Kwa mujibu wa baba huyo, mfanyakazi huyo alikuwa bado mgeni na mpaka anaondoka alikuwa ametimiza siku 14 tu. Hata hivyo, baba huyo aliongeza kuwa, mfanyakazi huyo alikamatwa maeneo ya Buzuruga jijini Mwanza akiwa na mtoto huyo na kwa sasa anahojiwa ili kujua lengo la kuondoka naye.

Note: Only a member of this blog may post a comment.